Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

UJUMUISHWAJI WA MASUALA YA JINSIA KATIKA SERA, SHERIA, MIPANGO NA PROGRAMMU MBALIMBALI KWENYE UTUMISHI WA UMMA NI HATUA MUHIMU KUFIKIA UIMARISHWAJI WA USAWA WA KIJINSIA


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Wakurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara pamoja na Waratibu wa Jinsia Ngazi ya Wizara kuweka mbinu za kuimarisha mfumo wa utoaji haki, kudhibiti uonevu, dhuluma, unyanyasaji na unyonyaji wa kijinsia pamoja na kuingiza masuala ya jinsia katika Mipango, Mikakati na Programu ya Wizara zao ili kuleta maendeleo endelevu.

Bw. Daudi amesema hayo leo wakati akifungua semina elekezi ya Mwongozo wa Jinsia (2023) kwa Wakurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara pamoja na Waratibu wa Jinsia Ngazi ya Wizara katika ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.

Amesema kumekuwepo na viashiria na matukio mbalimbali ya kutowatendea haki baadhi ya watumishi kutokupata stahiki zao kwa wakati, kutopewa nafasi za kujiendeleza, kukataliwa uhamisho, kutopewa likizo na nauli ya likizo, madai ya muda mrefu kwa watumishi, na unyanyasaji na dhuluma za kijinsia mahali pa kazi, udhalilishaji na uonevu ambao kwa kiasi kikubwa umewafedhehesha watumishi na kutweza utu wao.

“Baadhi ya watumishi wamekuwa wakinyanyasika katika maeneo yenu ya kazi kwa kunyimwa haki zao za msingi, niwasisitize kusimamia jambo hili mara moja kwani mwisho wake watumishi hao watashindwa kufanya kazi zao kwa ukamilifu na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa letu,” Bw. Daudi amesisitiza.

Amesema ujumuishwaji wa masuala ya jinsia ni muhimu sana maana ni chachu na huleta ufanisi na tija katika utendaji wa kazi. Aidha, huwawezesha watumishi wanaume kwa wanawake kutumia ujuzi, vipaji na vipawa walivyonavyo kutekeleza majukumu yao na kuleta taswira njema katika taasisi zao.

Amesema Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha Usawa wa Kijinsia katika Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja kuweka mazingira wezeshi yanayozingatia mahitaji ya kijinsia na hatua za makusudi (affirmative actions) ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi na majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki katika  nafasi za  uongozi na maamuzi ili kuzifikia fursa na kujenga usawa kati ya wanawake na wanaume na kuwezesha utekelezaji wa lengo namba tano (5) la Malengo Endelevu ya Mwaka 2030 kufikia Usawa wa Kijinsia kwa asilimia 50.

Bw. Daudi ameishukuru Taasisi ya UONGOZI kwa kuendelea kutafsiri ndoto za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo kwa nyakati tofauti wameandaa programu za Uongozi kwa Wanawake awamu kwa awamu na kuwezesha kufanyika kwa Semina elekezi juu ya mwongozo wa ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma kwa Ngazi ya Wizara.

Semina hiyo ya siku mbili imeratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI.