Habari
“UJENZI WA OFISI YA TAKUKURU NYANG’HWALE NI UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM WA KUPAMBANA NA RUSHWA, HEKO KWA VIONGOZI WA OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA NA WATENDAJI WA TAKUKURU’’- Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imewapongeza Viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 kuhusiana na mapambano dhidi ya rushwa.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 14 Machi, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa ziara ya Kamati hiyo iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Mkoani Geita.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati yake, Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema CCM ilipokuwa inaomba kura kwa wananchi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 iliahidi mambo mengi ikiwemo kupambana na rushwa na kuitokomeza, jambo ambalo limetekelezwa kwa ufasaha kwa kujenga Ofisi za TAKUKURU katika maeneo mbalimbali nchini na kuanzisha klabu za wapinga rushwa mashuleni.
“Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza Ilani, tumeona Ilani imetekelezwa kweli kweli katika kuzuia na kupamba na rushwa. Chama kiliahidi, sisi kama Wabunge jukumu letu ni kukagua kuona imetekelezwaje, hapa tunaona ilani imetekelezwa kwa asilimia100 kwani tumeridhishwa na ujenzi huu wa Ofisi ya TAKUKURU Nyang’hwale,” ameongeza.
Mhe. Dkt. Ndumbaro ametoa maelekezo kwa Viongozi wa Ofisi hiyo kuendelea kusimamia ubora wa majengo yote yatakayojengwa na ujenzi wa ofisi zote za TAKUKURU nchini.
Akitoa maelezo ya awali ya utekelezaji wa mradi wa jengo la TAKUKURU Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameishukuru Kamati hiyo kwa maelekezo na miongozi mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyatoa na kufanikisha utekelezaji mzuri wa majukumu ya Ofisi anayoiongoza ikiwemo ujenzi wa jengo hilo la TAKUKURU.
Mhe. Kikwete amesema mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 386 ambapo utekelezaji wake ulifuata taratibu zote za manunuzi kwa kuongozwa na sheria ya manunuzi na umetekelezwa kupitia Force Account.
Mhe. Kikwete ameahidi kuendelea kutekeleza maelekezo yote ambayo yatatolewa na Kamati hiyo ili kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa maendeleo ya taifa.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa TAKUKURU, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila amesema tangu kuanzishwa kwake TAKUKURU imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa majengo lakini katika kutatua changamoto hiyo, Serikali imekuwa ikijitahidi kujenga na kutafuta majengo ya kupanga ili kutekeleza majukumu yake ya kuzuia na kupamba na rushwa.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka kipeumbele na kuchukua hatua mbalimbali ili kuiimarisha taasisi hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga majengo yenye miundombinu ya kisasa na kukarabati majengo ya zamani,” ameongeza Bw. Chalamila.
