Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

TATUENI CHANGAMOTO ZA WATUMISHI ILI WAWATUMIKIE WANANCHI KIKAMILIFU- Mhe.Simbachawene


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewasisitiza waajiri katika taasisi za umma kutenga muda wa kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi na kuzifanyia kazi kwa lengo la kuwapa ari ya kuendelea kuwahudumia wananchi kikamilifu.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na Viongozi wa Mkoa wa Tanga na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga, Mhe. Simbachawene amesema rasilimaliwatu ni rasilimali muhimu sana kuliko rasilimali nyingine yoyote katika kuleta maendeleo, hivyo wasipotatuliwa changamoto zao hakutakuwa na matokeo chanya.

“Utatuzi wa changamoto uwe ni ajenda ya kila siku, Viongozi wa ngazi za juu, RAS, DAS mpange ratiba ya kuwasikiliza watumishi na kujua changamoto walizo nazo na kuangalia namna bora ya kuzitatua. Iwapo mtafanya ziara za kuwasikiliza watumishi, ninaamini changamoto zitapungua na watumishi watatekeleza majukumu yao kikamilifu.” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Ameongeza kuwa, yeye pamoja na viongozi wengine wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wako tayari kushirikiana na Viongozi na Watendaji hao kutatua changamoto za watumishi na ndio maana wamekuwa wakifanya ziara za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini ili kusikiliza changamoto za watumishi hao na kuzitatua.

“Sisi viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tuko tayari kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto za watumishi, kwa hiyo kaeni na watumishi wenu ili mjue changamoto wanazokutana nazo na mzitatue, na zile zitakazohitaji ushiriki wetu msisite kutushirikisha ili tuzitatue kwa pamoja kwa lengo la kuwafanya watumishi hawa waweze kutoa huduma bora kwa wananchi” Mhe. Simbachawene ameongeza.

Aidha, Mhe. Simbachawene amewataka watumishi wa umma kufahamu kuwa utumishi wa umma unaendeshwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni,Taratibu na Miongozo, hivyo ni lazima watumishi watambue taratibu hizo wanapodai haki zao.

Amesema kuna changamoto mbalimbali zinazosababishwa na uzembe wa watendaji na nyingine watumishi kukosa uelewa wa taratibu za kiutumishi. Hivyo, ametoa rai kwa watumishi kusoma nyaraka za kiutumishi ili kujua wajibu na haki za watumishi.

Mhe. Simbachawene ameanza ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga ya kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi wa umma mkoani humo kwa lengo la kuzitatua pamoja na kukagua utekezaji wa miradi ya TASAF ambapo leo ameanza na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga.