Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

TASAF YAJENGA SOKO LA KISASA - MADABA


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapongeza wananchi wa kijiji  cha Lituta katika halmashauri ya Wilaya Madaba mkoa wa Ruvuma kwa kutoa ushirikiano hadi kujengewa Soko la Kisasa.
Mhe. Kikwete amesema kuwa mradi huo wa soko la kisasa uliombwa na wananchi wa Madaba kupitia kwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt. Joseph Mhagama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.

“Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora alipokea maombi yenu na akaridhia fedha zitengwe na hatimaye kupitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na Bunge kwa jumla ili kuondoa changamoto ya soko katika Kijiji cha Lituta” ameongeza Mhe. Kikwete 

Aidha, ujenzi wa Soko hili ni moja ya jitihada mahususi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwatoa wananchi katika wimbi la umaskini kwa kuwa wananchi watafanya biashara katika maeneo safi na wateja wataongezeka, hivyo kuinua uchumi wa wanamadaba.

Pia, amebainisha kuwa awali soko lilikuwa na hadhi ya chini na sasa wananchi wamepata visimba vya hali nzuri. Soko la awali lilikuwa  na vizimba 34 wakati la sasa lina vizimba 80. Usanifu na ujenzi umezingatia mahitaji ya sasa na ya baadae.

Hali kadhalika, Mhe. Dkt. Mhagama amewapongeza viongozi na watendaji wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuisimamia vizuri TASAF na kuhakikisha jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutafuta fedha na kuhudumia wananchi wake zinafanyika kwa ufanisi.