Habari
WAZIRI SIMBACHAWENE: TAPSEA CHAMA CHA KIPEKEE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amesema Chama Cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) ni Chama cha kipekee kinachokua na kuimarika haraka wakati kikizingatia misingi ya taaluma hiyo na weledi wa kazi.
Ameongeza kuwa, upekee wa chama hicho unaonekana kutokana na jitihada za viongozi wa chama kuhamasisha na kuunganisha wanachama kutoka sekta ya umma na binafsi.
Mhe. Simbachawene alisema hayo Mei 16, 2025 kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango kufungua Mkutano Mkuu wa Kumi na Mbili TAPSEA unaofanyika katika ukumbi wa Ngurudoto Wilaya ya Arumeru Jijini Arusha.
“Nimefurahishwa na mchanganyiko wa wanachama katika Mkutano huu wa Kumi na Mbili ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanachama kutoka madhehebu ya dini ambao wameongeza heshima kwa chama hiki” alisema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene amesema mkutano huo hufanyika mara moja kwa mwaka na hukutanisha wanachama wa TAPSEA ili kuwakumbusha masuala mbalimbali kuhusu taaluma yao na kubadilishana uzoefu.
Aidha, aliongeza kuwa kupitia mikutano kama hiyo, wanachama wanakumbushwa kuzingatia weledi wa kazi katika utendaji kazi ili kuondoa mianya ya uvujaji wa siri ambao unaweza kudhoofisha utendaji kazi, kuleta uhasama kati ya wajiri na watumishi, kuvuruga uhusiano mwema na hata kuhatarisha usalama wa Taifa.
Pia, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali watumishi hao ambapo amemtuma Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango ili kufikisha salaam zake muhimu na kufungua mkutano huo ambao umekutanisha zaidi ya washiriki elfu tano.
Mkutano huo wa TAPSEA kwa mwaka 2025 unaongozwa na kaulimbiu isemayo: Mwandishi Mwendesha Ofisi mwenye Weledi na Ari ya Mabadiliko ni daraja kati ya Teknolojia na Ufanisi wa Taasisi.