Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

TANZANIA NA OMAN ZAIMARISHA USHIRIKIANO USIMAMIZI KUMBUKUMBU NA NYARAKA KIDIJITALI


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea vifaa vya kisasa vya Chumba cha Kanzi Data, vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na miundombinu iliyoboreshwa ya mtandao kutoka Mamlaka ya Taifa ya Nyaraka na Kumbukumbu ya Sultanate ya Oman.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali katika mfumo wa kidijitali, kuongeza usalama wa taarifa za Serikali, kuboresha upatikanaji wa nyaraka kwa wakati, kuimarisha uhifadhi wa muda mrefu wa kumbukumbu muhimu za taifa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma.

Akizungumza Julai 15, 2026 jijini Dar es salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb), amesema msaada huo ni ishara ya uhusiano wa kihistoria na ushirikiano imara uliopo kati ya Tanzania na Oman.

Mhe. Kikwete amesema makabidhiano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) iliyosainiwa mwaka 2012 kati ya Tanzania na Oman kuhusu usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka. 

*“Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya nchi hizo mbili katika kuendeleza mageuzi ya kidijitali, kuhifadhi urithi wa nyaraka za Taifa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma. Uwekezaji katika miundombinu ya TEHAMA ni muhimu katika kuhakikisha uhalisia, uadilifu, usalama na uhifadhi wa muda mrefu wa kumbukumbu za umma sambamba na kulinda urithi wa taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo” amesema.*

Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Taifa ya Nyaraka na Kumbukumbu ya Sultanate ya Oman, Dkt. Hamad Al-Dhawyani, amesema Oman itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka kupitia kubadilishana uzoefu, mafunzo ya kitaalamu, tafiti, uhifadhi wa kidijitali na utekelezaji wa miradi ya pamoja itakayowanufaisha wananchi wa nchi zote mbili.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali za Tanzania na Oman, akiwemo Balozi wa Sultanate ya Oman nchini Tanzania, Mheshimiwa Said Hilal Al-Shidhani, Balozi Abdallah Kilima kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na viongozi na watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka.