Habari
SERIKALI YATOA VIBALI VYA AJIRA 86,500 KATIKA MWAKA WA FEDHA 2024/25 NA 2025/26

Tarehe 11.10.2025
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26, imetoa vibali vya ajira 86,500 ili kuhakikisha Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinakuwa na watumishi wa kutosha kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi kikamilifu.
Akizungumza na Vyombo vya Habari leo Oktoba 11, 2025 jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amesema ajira hizo zinahusu kada mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Kilimo, UhandisI na sekta nyingine.
Katibu Mkuu Mkomi amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali ilitoa kibali cha nafasi 45,000 za ajira mpya kwa Taasisi mbalimbali na utekelezaji wake ulianza tarehe 29 Aprili, 2025 na kufuatia kutolewa kwa kibali hicho, mchakato wa kujaza nafasi hizo umefanyika na hadi sasa nafasi 30,863 zimejazwa na wahusika wamepangiwa vituo vya kazi. Aidha, nafasi 6,701 usaili umefanyika na wahusika watapangwa vituo vya kazi ndani ya Mwezi Oktoba, 2025 na nafasi 7,436 ujazaji wake utakamilika Mwezi Novemba, 2025 na wasailiwa kupangwa vituo vya kazi mwezi huo huo.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali iliidhinisha nafasi 41,500 za ajira mpya kwa Taasisi mbalimbali zikiwemo nafasi 12,176 za Walimu na nafasi 10,280 za kada za Afya ambapo utekelezaji wake unaanza mara moja.
Kufuatia kutolewa kwa vibali hivyo, Katibu Mkuu Mkomi ameielekeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuanza mchakato wa kujaza nafasi hizo za mwaka 2025/26 pamoja na kukamilisha mchakato wa nafasi zote za Mwaka 2024/25.
Vile vile Bw. Mkomi ametoa maelekezo kwa waajiri wote kutoa ushirikiano kwa Sekretarieti ya Ajira ili kuhakikisha lengo la ujazwaji wa nafasi za ajira linatimia.
“Ili kuhakikisha Sekretarieti ya Ajira inatekeleza jukumu hili ipasavyo, ninawaelekeza Waajiri kutoa ushirikiano. Aidha, ninawaelekeza Waajiri ambao Sekretarieti ya Ajira imekasimu madaraka ya uendeshaji wa mchakato wa ajira kwa baadhi ya kada, kuhakikisha wanaendesha usaili huu mara moja ili kujaza nafasi walizoidhinishiwa kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni za uendeshaji wa usaili katika Utumishi wa Umma,” Katibu Mkuu Mkomi amesisitiza.
Katika kuhakikisha gharama za kufanya usaili zinapungua na unafanyika kwa wakati, Bw. Mkomi ameielekeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuwa zoezi la usaili lifanyike kila Mkoa Tanzania Bara na vituo vilivyoandaliwa mahsusi wa upande wa Zanzibar ili kutoa fursa kwa waombaji kutoka katika maeneo husika kuomba na hatimaye kusailiwa
Pia amesema waombaji watakaofaulu usaili lakini wakashindwa kupangiwa kazi baada ya usaili wawekwe katika kanzidata na waendelee kupangiwa kazi kwa kadri nafasi za ajira mpya zitakapokuwa zinapatikana.
Amesema waombaji hao watapangiwa kazi katika Taasisi zitakazokuwa na nafasi popote hapa nchini na kuongeza kuwa barua za kupangiwa vituo vya kazi kwa wasailiwa watakaofualu usaili zipatikane katika “Mfumo wa Ajira Portal” kupitia akaunti za wahusika.
Katibu Mkuu Mkomi ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kutoa vibali vya ajira kulingana na mahitaji ya sekta mbalimbali ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi zinapatikana.