Habari
SERIKALI YAKUSUDIA KURATIBU GAZETI LA SERIKALI KIDIJITALI

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amesema katika kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya TEHAMA Serikalini, Ofisi hiyo imesanifu na kujenga Mfumo wa Kidijitali utakaowawezesha wadau wa Gazeti la Serikali kuwasilisha taarifa zao kwa njia ya kielektroniki.
“Sasa hivi tuko kwenye ulimwengu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ambapo Serikali yetu kupitia Viongozi Wakuu, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akihimiza mara kwa mara matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi ili kupunguza mianya ya rushwa na gharama, hivyo tunaamini kupitia Mfumo, tutaboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.’’ Amesema Bw. Mkomi.
Bw. Mkomi ameongeza kuwa, Mfumo huo utawawezesha wadau wa Gazeti la Serikali kupata huduma kwa njia ya kielektroniki ambayo ni rahisi, haraka na yenye gharama nafuu itakayowawezesha kuwasilisha taarifa zao zitakazochapishwa na kupatikana kwa Gazeti hilo.
“Sote tunafahamu umuhimu wa Gazeti la Serikali kwa wadau mbalimbali hapa nchini hivyo, kuuboresha mfumo huu kutasaidia sana wadau wetu kuwasilisha taarifa zao kwa haraka na kupunguza malalamiko kama sio kuyaondoa kabisa” Amesisitiza Bw. Mkomi.
Amesema baada ya Ofisi yake kusanifu na kujenga mfumo huo ambao bado ni rasimu, waliona ni vema wakawashirikisha wadau ili kupata maoni yao. Ni matumaini yangu kuwa, kupitia kikao hiki, maoni mbalimbali yatapatikana ili kuboresha mfumo huo ambao ni muhimu kwa wadau wa Gazeti la Serikali.” Bw. Mkomi amesisitiza.
Aidha, ameongeza kuwa, kupitia mfumo huo, taarifa zitahaririwa na kupelekwa kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa njia ya kielektroniki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Mary Mwakapenda amewashukuru wadau hao kwa kuitikia wito katika kikao kazi hicho pamoja na maoni mengi waliyoyatoa ambayo yatasaidia katika kuboresha na kuongeza tija katika utekelezaji wa Mfumo huo.