Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAJIVUNIA MAFANIKIO LUKUKI KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MINNE YA UONGOZI WA RAIS MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne imepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali.

Amesema mafanikio haya yanatokana na azma ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuujenga Utumishi wa Umma kuwa wenye tija katika maendeleo ya taifa.

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo tarehe 17 Aprili, 2025 wakati akizungumza na vyombo vya habari kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO Jijini Dodoma.

Ameyataja miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na

kusimamia Mikataba ya Utendaji Kazi Serikalini ambapo Serikali ilijenga mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (e-UTENDAJI - PEPMIS/PIPMIS) unaotumika kusimamia utendaji kazi wa watumishi wa umma na taasisi za umma ili kuwezesha kubaini kiwango cha utendaji kazi na uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma.

Kusimamia Mipango na Uendelezaji Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma baada ya kuona kuna tatizo la upungufu wa watumishi katika maeneo mengi, ilitafuta namna bora ya kuondoa changamoto hiyo kwa kujenga Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu (HR-Assessment).

“Mfumo huu wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ni msaada mkubwa kwani unabainisha idadi ya watumishi walioko katika kila kituo cha kazi na upungufu au ziada iliyopo ili kuwa na idadi ya watumishi sahihi katika sehemu sahihi za utekelezaji wa majukumu yao.” ameeleza Mhe. Simbachawene

Katika eneo la Usimamizi wa Maslahi na Stahiki za Watumishi wa Umma Mhe, Simbachawene amesema, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyaangalia maslahi ya watumishi wa umma kwa jicho la pekee ikiwemo kupunguza kodi ya mapato (PAYE) kutoka 9% hadi asilimia 8%, kufuta tozo (retention fee) ya 6% iliyokuwa ikitozwa kutoka katika mishahara ya watumishi wa Umma walionufaika na Mikopo ya Elimu ya Juu, kulipa malimbikizo ya mshahara, kupandisha vyeo, kubadilisha kada pamoja na kuundwa kwa Mfumo wa Huduma Mtandao kwa Watumishi (Watumishi Portal) unaowawezesha Watumishi wa Umma kupata huduma mbalimbali za kiutumishi moja kwa moja bila kulazimika kwenda kwenye Ofisi za Waajiri wao.

Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2025 madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 148,137 yenye jumla ya Sh. 248,528,998,254.79 yalipokelewa na kushughulikiwa. Aidha, katika kipindi hicho, madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wastaafu 10,022 kutoka kwa waajiri yenye jumla ya Sh. 33,290,109,780.75 yamepokelewa na kushughulikiwa na wahusika wamelipwa kupitia kwa waajiri wao.

Ameongeza kuwa mpaka kufikia tarehe 31 Machi, 2025 Jumla ya watumishi wa umma  610,733 wamepandishwa vyeo, 42,515 wamebadilishwa kada, 3,208 wamepata uteuzi, 157,512 wamesafishiwa taarifa zao za kiutumishi, 10,725 wamebadilishiwa vyeo, 3,877 wamerekebishiwa majina, 9,269 wamefanyiwa mabadiliko ya mshahara binafsi, 2,558 wamerejeshwa kwenye utumishi wa umma na 133,317 wameajiriwa katika Taasisi mbalimbali za umma. Aidha, katika kipindi hicho, Jumla ya nafasi za ajira 155,008 zimetolewa na jumla vibali vya ajira mbadala 41,673 vimetolewa ili kujaza nafasi zilizobaki wazi kwa sababu mbalimbali.

Mhe. Simbachawene amesema, Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha miaka minne yameonekana pia kwa upande wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF) kwani, Mpango wa Miradi ya Kutoa Ajira za Muda kwa Walengwa kufikia Desemba, 2024, jumla ya miradi 27,863 ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imetekelezwa.

Kwa upande wa TAKUKURU, Mhe. Simbachawene amesema, TAKUKURU imetekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini ambapo Programu ya TAKUKURU Rafiki ilizinduliwa ili kuleta mafanikio makubwa na kero nyingi zilizoibuliwa zilitatuliwa ikiwamo sekta za afya, elimu, maji, nishati, mawasiliano, maendeleo ya jamii, mazingira, ujenzi, ardhi, kilimo, ufugaji, usafirishaji, usalama na haku jinai, hivyo kuzuia vitendo vya rushwa na kuboresha huduma zinazotolewa kwa umma.

Waziri Simbachawene ameongeza kuwa, katika kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kidijitali, Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imetekeleza agizo la Mhe. Rais kwa kujenga na kusanifu mfumo wa pamoja wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus-GovESB) ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi sambamba na kupunguza mianya ya rushwa, kuondoa urasimu na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali,

Aidha, katika kutengeneza Mfumo shirikishi utakaowezesha Mifumo ya Taasisi kuwasiliana na kubadilishana taarifa, mifumo 202 ya taasisi za umma 179 imeunganishwa na inabadilishana taarifa ikiwemo Taasisi za Sekta ya Haki Jinai zinazojumuisha Mahakama, TAKUKURU, Polisi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Mhe. Simbachawene amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo na kusimamia kikamalifu kuhakikisha yametekelezwa kwa ufanisi.