Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

SERIKALI KUONGEZA BAJETI KUHIFADHI NYARAKA ZA VIONGOZI KIDIJITALI


 

 

Serikali imedhamiria kuja na mpango mkakati wa kuongeza bajeti itakayosaidia katika suala la kuhifadhi na kutunza kumbukumbu na nyaraka za viongozi mbalimbali wa serikali kwa njia ya tovuti. 

 

Hayo yamesema na Waziri wa Nchi Ofisi Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. 

 

Simbachawene amesema kuongezwa kwa bajeti ya kuhifadhi nyaraka kwa njia ya kidijitali itasaidia vijana na Watanzania kwa ujumla kuweza kusoma na kujua historia ya nchi yao na Bara la Afrika kupitia viongozi wao.

 

Aidha ameeleza kuwa Serikali iko vizuri katika eneo la kuhifadhi nyaraka na tayari ofisi ya Kumbukumbu na Nyaraka ilishajengwa jijini Dodoma kwa ajili ya kuweka nyaraka hizo kwa njia ya machapisho na kidijitali. 

 

Mhe. Simbachawene amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wa Viongozi Wastaafu waliolitumikia taifa kwa muda mrefu na kuweza kutoa maelekezo ya kushirikiana na familia ya Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim kukusanya nyaraka na kufanikisha uzinduzi wa tovuti hiyo.

 

“Mhe. Rais, tunashukuru kwa maelekezo yako uliyoyatoa kupitia Katibu Mkuu Kiongozi ambaye aliyasimamia kikamilfu na kuweza kufanikisha, hili ni tukio la kihistoria na linatupa funzo kuwa jambo hili linaweza kufanyika kwa Viongozi Wastaafu wengine,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

 

Mhe. Simbachawene amebainisha kuwa ushirikiano wa familia ya Dkt. Salim Ahmed Salim umekuwa na mchango mkubwa katika kupatikana kwa taarifa za kiongozi huyo ili ziweze kuhifadhiwa kwenye Tovuti maalum kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

Ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa viongozi kujenga utaratibu wa kupeleka taarifa zao Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa iliyopo jijini Dodoma ili taarifa zao ziweze kuhifadhiwa kidigitali kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye.