Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

SERIKALI KUJENGA UTUMISHI WA UMMA WENYE UFANISI, UWAJIBIKAJI NA KUONGEZA FURSA ZA AJIRA NA USTAWI WA VIJANA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali kupitia Ofisi yake inaonesha dhamira thabiti ya kujenga Utumishi wa Umma wenye ufanisi, uwajibikaji na unaozingatia misingi ya utawala bora ili kwenda sambamba na matarajio ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Waziri Kikwete amesema hayo wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es salaam Desemba 12, 2025. Mkutano huo ulilenga kutoa taarifa ya namna Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inavyotekeleza wajibu wake kwa Taasisi za umma, Watumishi wa Umma na Wananchi kwa jumla.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, dhamira hiyo imeweka vipaumbele ambavyo ni kuongeza fursa za ajira na ustawi wa vijana wa kitanzania, maboresho ya mifumo ya ajira, utoaji wa huduma, mafunzo ya kujenga uwezo, usimamizi wa rasilimaliwatu pamoja na kuimarisha mifumo ya mawasiliano kati ya Serikali na wananchi.

Mhe. Kikwete alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha nafasi za ajira katika Utumishi wa Umma zinakuwa za wazi na ushindani kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (PSRS) ili kuwajengea Watanzania imani na uaminifu kwa Serikali yao kwa ustawi wa Taifa.

Vile vile, Mhe. Kikwete amesema, kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeelekeza Sekta ya kipaumbele iwe na uwezo wa kuzalisha ajira na kuongeza fursa ya ajira kwa vijana, kuongeza kipato kwa wananchi na kupunguza umaskini kwa kuzingatia viwango vya juu vya weledi unaopatikana na kufuata misingi ya haki, umahiri na utendaji bora.

Aidha, Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, katika kufanikisha maelekezo ya Dira 2050, kupitia Serikali kwa mwaka wa Fedha 2025/26 kibali cha nafasi 41,500 za ajira zikiwemo nafasi 12,000 za ajira ambazo ni ahadi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoahidi kutoa nafasi 5,000 za kada za Afya na nafasi 7,000 za Walimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati ambazo ni uzalishaji wa ajira zilizo rasmi ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani.

Mhe. Kikwete amesema kuwa, ili kuhakikisha usaili unafanyika kwa wakati na kwa lengo la kuongeza ufanisi, usaili wa mchujo wa nafasi hizo utafanyika kwa kutumia mfumo wa kieletroniki uitwao “Online Aptitude Test (OATS)” na utafanyika katika vituo mbalimbali kama vile Taasisi za Elimu ya Juu, Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi (VETA) na Shule za Sekondari zenye maabara za Komputa zinazopatikana katika mikoa yote na Vituo mahsusi kwa Unguja na Pemba.

“Mhe. Rais Dkt. Samia aliahidi baada ya kuingia madarakani atatoa nafasi 5,000 za kada za Afya na nafasi 7,000 za Walimu ndani ya siku 100 na tayari nafasi za ajira 12,000 zimeshatangazwa na waombaji wenye sifa wameitwa kwenye usaili utakaofanyika kuanzia tarehe 13 Desemba, 2025 katika mikoa yote Tanzania Bara na Vituo mahsusi kwa Unguja na Pemba,” Amefafanua Mhe. Kikwete.

Pia, Waziri huyo aliwaomba wandishi wa habari kuendelea kuwahabarisha na kuwaelimisha Watanzania hususan vijana, kutambua fursa zilizopo na kuzitumia kwa manufaa ya taifa. Utambuzi huo unaifanya Serikali kuendelea na jitihada zake za kukuza ujuzi, kuhimiza maadili, kupanua fursa za makazi bora na kuandaa vijana wa Kitanzania ili kukabiliana na uchumi wa kidijiti.