Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

SERIKALI KUIMARISHA UFANISI WA UTENDAJI KAZI  KUPITIA UJENZI WA OFISI ZA TAKUKURU


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema uzinduzi wa jengo la TAKUKURU katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ni hatua muhimu inayothibitisha dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha mazingira ya utendaji kazi, kuongeza ufanisi pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi ili kuleta Maendeleo ya Watanzania.

Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo Mkoani Pwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wakati akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU ambalo litaboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa TAKUKURU ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Mhe Kikwete amesema kuwa, Serikali imewawezesha TAKUKURU kwa kiwango kikubwa sana hivyo amewaasa kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii na weledi zaidi ili dhamira ya Serikali ya kuitokomeza rushwa nchini pamoja na maono ya TAKUKURU ya kuwa na Tanzania isiyo na rushwa yaweze kufikiwa.

Vilevile, Mhe. Kikwete ametoa wito kwa Watumishi wa TAKUKURU Chalinze pamoja na Mikoa na Wilaya ambazo kuna majengo mapya kutunza na kuthamini majengo hayo pamoja na vitendea kazi vyote vilivyomo ili viweze kutumika hata na vizazi vijavyo.

Aidha, ametoa wito kwa taasisi ya TAKUKURU, Sekta za Umma na  Watanzania wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha fedha za Serikali zinazotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri zinatumika kulingana na malengo yaliyowekwa.

Amesema, utaratibu huo ni muhimu katika kuongeza uwazi na uwajibikaji na hivyo kuziba mianya ya rushwa na kuongeza ushiriki wa Wananchi katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa ipasavyo.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Kikwete amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila pamoja na watendaji wa taasisi hiyo kwa uadilifu na weledi unaoonekana katika usimamizi wa ujenzi wa jengo hilo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye ujenzi wa majengo katika wilaya na mikoa mbalimbali nchini na hii ni kuonesha utashi wa Mhe. Rais katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.