Habari
SERIKALI KUBAINI MWENENDO WA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI WA UMMA
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi, amewataka Vinara wa Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma PEPMIS kujitoa wakati wote kuwaelekeza watumishi wengine katika maeneo yao ya kazi ili Serikali iweze kubaini mwenendo halisi wa utendaji kazi wa watumishi wa umma.
Bw. Daudi, amesema hayo leo Mei 8, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Vinara takribani 110 wa Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma kutoka katika taasisi mbalimbali za umma zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Aidha, amewapongeza Vinara hao kwa kuchaguliwa na kupata fursa ya kujengewa uwezo ili kwenda kuwasaidia watumishi wengine katika taasisi mbalimbali zilizopo katika mikoa yao.
Pia, amewasisitiza Vinara hao kutambua kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewaamini na kuwapa dhamana kubwa ya kutoa msaada wa kiufundi kwa watumishi wengine katika masuala ya matumizi ya mfumo wa PEPMIS. Hivyo, wanatakiwa kutumia dhamana hiyo kwa ufanisi.
“Ninatambua mafunzo kama haya yalitolewa kwa watumishi wote katika kipindi cha mafunzo ya awali na ninyi mkiwa ni sehemu ya washiriki hao, sasa mumechaguliwa kuwa vinara kutokana na uwezo wenu, shauku na mapokeo chanya ya matumizi ya mifumo hii, hivyo jitoeni zaidi na muwe sehemu ya watumishi watakaotambuliwa na Serikali na vizazi vijavyo kuwa sehemu ya waliofanya mageuzi katika utumishi wa umma” amesisitiza Bw. Daudi.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mikataba ya Utendaji Kazi, Ofisi ya Rais UTUMISHI Bi. Elizabeth Makyao amesema Mifumo ya PEPMIS na PIPMIS ni mipya na inahitaji wataalamu wengi ambao wanauwezo wa kutoa msaada wa kiufundi kwa ukaribu, haraka na ufanisi ili kuondoa changamoto ya kutafuta msaada huo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iko tayari kupokea jambo ambalo litakuwa nje ya uwezo wao na kusaidia kupata ufumbuzi wa haraka kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, mafunzo hayo ya siku tatu ni matokeo ya mapendekezo ya Timu ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora walioshiriki kutoa na kusimamia mafunzo ya PIPMIS na PEPMIS kuanzia Novemba 23, 2023 hadi Februari 15, 2024 katika taasisi zote za umma zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara.