Habari
SAYANSI NA TEKNOLOJIA YASUKUMA MABORESHO YA KANUNI ZA KUDUMU KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - UTUMISHI SACP. Ibrahim Mahumi amesema Serikali imeamua kufanya mapitio na maboresho makubwa ya kanuni za kudumu katika Utumishi wa Umma kutokana na mabadiliko na ukuaji wa sanyansi na teknolojia ambayo imeathiri eneo la Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.
SACP. Mahumi alisema hayo Oktoba 2, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Jijini Dodoma wakati wa kufungua kikao kazi cha Wadau cha kuhakiki rasimu ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma Toleo la Nne la mwaka 2025. Kikao kazi hicho kilihusisha Wakurugenzi na Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka katika taasisi mbalimbali za umma.
“Mwitiko huu ni ishara tosha kuwa maoni thabiti yatapatikana kwa kuzingatia kuwa ninyi ndio mnaopata changamoto wakati wa utekelezaji wa kanuni hizi, hivyo maoni yenu kama wadau ni muhimu katika kuboresha Kanuni hizi za kudumu katika Utumishi wa Umma” alisema SACP. Mahumi.
SACP. Mahumi alisema kuwa kwa sasa kuna sheria nyingi zinazosimamia maeneo ya Utumishi wa Umma ikiwemo Sheria ya Utumishi wa Umma, Sheria ya Mahusiano Kazini, Sheria za hifadhi ya jamii hivyo mawazo yenu yanatakiwa kuleta muunganiko mzuri kati ya Sera, Sheria na Kanuni za kudumu katika Utumishi wa Umma.
Aidha SACP. Mahumi alisisitiza wadau hao kutoa maoni kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya 2050 ili kuwa na muunganiko wa kanuni hizo na kuleta urahisi kwa watumishi wa umma hasa pale wanapofanya marejeo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cyrus Kapinga amehitimisha mjadala huo kwa kuwashukuru washiriki wa kikao hicho kwa mawazo waliyotoa na kuahidi kuwa yote yaliyojadiliwa yamepokelewa na yatafanyiwa kazi.