Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

RIDHIWANI: SERIKALI YALIPA ZAIDI YA BILIONI 24 MADAI YA WATUMISHI AONYA WATUMISHI WANAOGHUSHI BARUA ZA UHAMISHO, ASEMA 6 MBARONI KESI UHUJUMU UCHUMI


Serikali imeendelea kuboresha ustawi wa watumishi wa umma kwa kulipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya Tsh. Bilipni 24,699,256,645.7 na kulipa watumishi 1,249 waliokoma utumishi yenye thamani ya zaidi ya Tsh. Bilioni 5,548,386,177.90.

Hayo yamebainishwa Juni Mosi, 2026 Mabele Hall jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) katika ufunguzi wa kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Wizara na Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mtaa.

Pamoja na maboresho hayo, Mhe. Ridhiwani amesema  wapo baadhi ya waajiri ambao hawatekelezi ipasavyo wajibu wao katika kushughulikia madai ya aina hiyo ambapo hadi kufikia Mei 28,2026 madai ya watumishi 18,021 yenye jumla ya Shilingi 50,917,523,216 hayajawasilishwa Ofisini kwake.

“Baadhi ya waajiri wamekuwa wakiwasilisha katika Ofisi hii madai yenye kasoro ambazo walipaswa kuzibaini kabla hawajayawasilishwa.  Vile vile, yapo madai ya malimbikizo ya mshahara yanayotokana na waajiri kutozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu na hivyo kuzalisha madeni makubwa kwa Serikali” amesema.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ridhiwani ametoa onyo kali kwa waajiri na viongozi wa taasisi za umma wanaokiuka sheria na taratibu za kiutumishi hususani kwa Waajiri kuchagua aina ya watu wa kufanya nao kazi, kutopokea watumishi wanaohamishiwa kwenye Taasisi zao, Waajiri kujimilikisha Taasisi na kuficha barua zenye maelekezo mahsusi ikiwemo barua za uhamisho.

Sambamba hayo, amesema Ofisi yake kwa kushirikiana na Taasisi za Haki Jinai imeanza kuchukua hatua mbalimbali kwa watumishi wanaojihusisha na ukiukwaji wa maadili ikiwemo kughushi barua za Ofisi hiyo ambapo hadi sasa jumla ya watuhumiwa Sita wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya Uhujumu Uchumi na kesi zinaendelea.

Awali akizungumza Katibu Mkuu Ofisi hiyo Juma Mkomi, amesema kikao hicho kimeandaliwa mahsusi kwa lengo la kutathmini nafasi ya wasimamizi wa Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, kubadilishana uzoefu katika kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali hususan katika Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma hasa tunapoelekea kwenye utekelezaji wa Dira Mpya ya Taifa ya 2050.

Pia, Mkomi  amesema kikao hicho kitajikita  zaidi katika kujadili masuala muhimu ya Usimamizi wa Utumishi wa Umma, Usimamizi  na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA Serikalini, changamoto zilizopo katika utekelezaji wa majukumu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu na namna bora ya kukabiliana nazo.

Kikao kazi hicho kina kauli mbiu isemayo “Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Sikivu, Jumuishi, Wenye Matokeo na Uwajibikaji kuelekea Dira 2050”.