Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

RAIS SAMIA ATOA AGIZO LA KUWASIMAMIA MABARAZA YA WAFANYAKAZI, YAONGEZA MISHAHARA 35%


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene kuendelea kusimamia mabaraza ya wafanyakazi  ili yaendelee kutimiza majukumu yake katika mahali pa kazi 

Mhe.Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kitaifa yamefanyika Mkoani Singida

Amesema uimara wa vyama vya wafanyakazi nchini ni muhimu katika kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi mahali pa kazi huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyama hivyo kwa kutimiza matakwa yao.

" Waziri ahakikishe anayasimamia  mabaraza haya ya wafanyakazi ili yaendelee kufanya kazi kwa ufanisi, ili yawe chombo cha kusaidia mawasiliano kati ya serikali na wafanyakazi." Amesisitiza 

Katika hatua nyingine, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  ametangaza nyongeza ya mshahara wa kima cha chini kwa asilimia 35 kwa watumishi wa umma, hatua inayotarajiwa kuinua kipato cha wafanyakazi wengi nchini.

Tangazo hilo linakuja wakati Serikali ikijitahidi kukabiliana na changamoto ya mfumuko wa  bei  huku kukiwa na nyongeza kubwa zaidi ya mshahara tangu mwaka 2020.

Katika maadhimisho hayo ya mwaka huu  2025 yenye Kauli mbiu isemayo: Uchaguzi Mkuu 2025: Utuletee viongozi wanaojali haki na masilahi ya

wafanyakazi, sote tushiriki,  Watumishi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora wameahidi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu huo  unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.