Habari
RAIS MHE.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUFUATA NYAYO ZA HAYATI MORINGE SOKOINE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka Watumishi wa Umma kutanguliza mbele uzalendo muda wote wanapokuwa ndani na nje ya utumishi wao huku akisisitiza kuwa Mtumishi wa umma muadilifu ni rahisi sana kuonekana na kutambulika kama ambavyo hivi sasa Waziri Mkuu wa zamani Hayati Edward Moringe Sokoine anatambulika kutokana na uzalendo na uadilifu wake
Rais Mhe.Dkt.Samia ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa hafla ya kuzindua Kitabu kinachohusu Maisha na Uongozi wake Hayati Edward Moringe Sokoine kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Hayati Sokoine alikuwa mfano na kiongozi aliyejali uwajibikaji, haki na uwazi. Aliamini katika dhana ya utumishi wa umma akitambua kwamba uongozi ni jukumu la kutumikia wananchi, kwa moyo wa kujitolea, akijenga nidhamu ya utendaji kazi ndani ya serikali, akisisitiza utumishi bora uadilifu na ufanisi katika kila hatua ya maendeleo.
“Leo tunapoangalia historia na mchango wake tunapata somo kubwa namna ya kiongozi wa kweli anavyoweza kuacha alama isiyofutika, juu ya kitabu hiki kizazi cha sasa na baadaye kitajifunza juu na maono na fikra za kiongozi huyu ambaye alikuwa mfano wa kuigwa katika siasa za Tanzania,”
"Niwashukuru familia ya Sokoine, maisha ya ndani kufikishwa kwa kiongozi huyu na wadau wa maendeleo kusoma kitabu hiki kuboresha utendajii wa kazi ili kuleta maendeleo na kufanikisha uchumi wa nchi. Huu ni urithi wa thamani utakaodumu vizazi na vizazi,”
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Waziri Mkuu wa zamani Hayati Edward Moringe Sokoine ameacha alama kubwa katika uongozi wake na atakumbukwa na vizazi hata vizazi kutokana na mambo mbalimbali aliyofanya ikiwemo kujenga nidhamu katika Utumishi wa Umma
Amesema Hayati Sokoine alikuwa ni Kiongozi aliyejali uwajibikaji, uadilifu na ufanisi katika kila hatua ya maendeleo na aliyeongoza kwa maadili mema, maono na aliyezingatia usawa kwa watu wake
Aidha, Mhe. Simbachawene ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa Watumishi wa Umma, Wadau wa Maendeleo pamoja na Watanzania wote kusoma Kitabu cha Maisha na Uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine ili kupata mafundisho yatakayosaidia kuboresha utendaji wao wa kazi na hatimaye kuleta maendeleo na kuimarisha ustawi wa Taifa