Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAMPONGEZA MTUMISHI WAKE KWA KUIBUKA KIDEDEA KATIKA MBIO ZA BAISKELI


Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imempongeza mtumishi wa ofisi hiyo, Bw. Omari Ligoneko kwa  kuibuka  mshindi wa kwanza  kwenye mchezo wa mbio za baiskeli kwenye  mashindano ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yaliyomalizika hivi karibuni Mkoani Iringa.

Aidha katika mashindano hayo, Ofisi hiyo  iliibuka mshindi wa nne kwenye mbio za mita 100 na mshindi wa tano  mbio za mita 200.

Akitoa pongezi hizo, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, UTUMISHI, ACP Ibrahim Mahumi amesema Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora inajivunia kwa ushindi huo ambao ni heshima kubwa kwao. 

"Mimi pamoja na Wajumbe wa Menejimenti tumeona ni vema tukakuita ili tukae pamoja na kukupongeza kwani tumetambua mchango wako ambao umeiletea heshima Ofisi,” Bw. Mahumi amesema.

Awali, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI, Bw. Musa Magufuli amempongeza Bw.Ligoneko na kuahidi kuwa ofisi yake itaendelea kujiimarisha zaidi katika michezo ili kipindi kijacho iweze kutwaa vikombe vingi zaidi.

“Mwaka huu licha ya kubeba kikombe kimoja lakini tumejitahidi sana ukilinganisha na miaka mingine, tumejipanga tutaanza mazoezi mapema ili mwakani tunyakue vikombe vingi zaidi,” Bw. Magufuli ameongeza.

Kwa upande wake, Mshindi huyo, Bw. Omari Ligoneko ameishukuru Menejimemti kwa kumpa heshima hiyo ya kuwa pamoja naye licha ya majukumu mengi yanayowakabili.

‘’Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Uongozi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kutupatia kibali cha kushiriki michezo ya SHIMIWI na Timu nzima ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa ushirikiano waliouonyesha  wakati wote wa michezo na hatimaye kuweza kuibuka mshindi wa kwanza katika mbio za baiskeli,” Bw. Ligoneko amesema.