Habari
OFISI YA RAIS - UTUMISHI YAENDELEA KUTOA MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WAKE IKISISITIZA UTOAJI WA HUDUMA BORA
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeendelea kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi wa ofisi yake kwa lengo la kuboresha utendaji kazi ili kuwawezesha watumishi hao kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau mbalimbali wa Serikali.
Akiwasilisha mada kuhusu Huduma kwa Mteja, Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Emmanuel Luvanda amesema malengo ya Utumishi wa Umma ni kuwahudumia wananchi kwa kiwango cha hali ya juu, hivyo kila mtumishi ni vizuri akawajibika kikamilifu ili kufikia malengo hayo.
Bw. Luvanda ameongeza kuwa, kwa kuendelea kuwajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora kwao kunawafanya wawe na imani kubwa na Serikali yao.
Aidha, Bw. Luvanda amewashauri watumishi wa Ofisi hiyo kutumia changamoto mbalimbali kama fursa ya kujifunza na kuona namna ya kutatua changamoto hizo na kuleta maboresho yenye ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa Magufuli ametoa wito kwa watumishi wa ofisi hiyo kuwahudumia wadau wote wanaohitaji huduma katika ofisi hiyo kwa kuzingatia misingi ya huduma bora ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kujenga taswira nzuri ya ofisi.
Mafunzo hayo elekezi ni utaratibu uliowekwa na Ofisi hiyo kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya Utumishi wa Umma ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.