Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA YAWAASA WATUMISHI WA UMMA KUACHA KUCHEZA KAMALI


Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imesema sio maadili kwa Watumishi wa Umma kucheza kamali ikwemo michezo wa kubashiri (betting) kwani inatweza utumishi wao katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Juni 28, 2024 katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamzi wa Maadili, Bw. Ally Ngowo wakati wa utoaji wa Semina ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Ofisi hiyo mahali pa kazi

Amesema Mtumishi wa Umma ni kioo katika jamii hivyo kujihusisha kucheza kamali kunapelekea Mtumishi kushindwa kuwahudumia wananchi na wakati mwingine kupata msongo wa mawazo endapo atapoteza fedha kwenye kamari

Katika hatua nyingine, Bw. Ngowo amesema sio maadili kwa Watumishi wa Umma kukopa fedha bila mpangilio.

Amefafanua kuwa baadhi ya watumishi wamekuwa wakikopa pasipokuwa na malengo, hivyo wakijikuta na madeni mengi yasiyokuwa na ulazima, hali inayowafanya kushindwa kufanya kazi zao ipasavyo.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Saikolojia, Dkt. Chris Mauki amesema katika maisha ya kila siku mabadiliko hayaepukiki na kama hawatayakubali mabadiliko hayo ni lazima watumishi wapate changamoto ya afya ya akili.

"Miili yetu haijaumbwa kupokea mabadiliko yanayotokea katika maeneo yetu ya kazi na maisha kwa ujumla na hivyo tumejikuta tukipata changamoto ya afya ya akili " amesema Dkt. Chris Mauki

Amesema kiasili binadamu wote ni woga wa mabadiliko na hiyo imepelekea binadamu kupambana na mabadiliko yasitokee hali inayopelekea kujikuta kwenye msongo wa mawazo na muda mwingine kupata matatizo makubwa.

Awali Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, SACP. Ibrahim Mahumi amesema mafunzo hayo yameletwa kwa vile Watumishi wa Ofisi hiyo wana kazi nyingi ambazo zimekuwa zikiwaletea msongo wa Mawazo hivyo mafunzo ni muhimu ili waweze kuwa wastahimilivu.

‘’Hapa kuna msongo wa mawazo sana hivyo mafunzo haya ya afya ya akili ni muhimu ili kuweza kuepukana nayo’’ amesisitiza Kaimu Katibu  Mkuu, SACP. Ibrahim Mahumi

Naye Daktari Bingwa wa Macho, Joshua Yeuze kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa akiwasilisha mada kuhusu Magonjwa Sugu yasiyoambukiza (Sukari na Presha ya Macho) akitoa semina ya magonjwa hayo amewaasa Watumishi wa Umma kujenga utamaduni wa kupima angalau kwa mwaka mara moja ili kujua hali za afya zao

‘’Hakikisheni mnafanya mazoezi mara kwa mara pamoja na kula chakula bora ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza’’ amesema Dkt. Yeuze

Katika hatua nyingine Mchunguzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Stephew Agwanda wakati akiwasilisha mada kuhusu Mkakati wa Taifa dhidi ya Rushwa amewaasa Watumishi hao kujiepusha vitendo vya rushwa mahali pa kazi