Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

OFISI YA RAIS-UTUMISHI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA SEKTA YA AFYA KATIKA KUHAKIKISHA WATUMISHI WA UMMA WANAPATA FURSA YA KUTAMBUA HALI ZAO ZA KIAFYA ILI KUONGEZA UFANISI KIUTENDAJI


Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya ikiwemo Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa ili kuhakikisha watumishi wa umma wanapata fursa ya kutambua hali zao za kiafya na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kuongeza ufanisi kiutendaji.

Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu - UTUMISHI ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Bw. Cyrus Kapinga wakati akizindua kambi maalum ya uchunguzi wa Magonjwa Yasiyoambukizwa kwa watumishi wa umma uliofanyika katika jengo dogo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mtumba jijini Dodoma.

Bw. Kapinga amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora ambayo ndio msimamizi wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina wajibu wa kuhakikisha Taasisi za Umma zinatekeleza dhana ya Utawala Bora ikiwemo kusimamia vema eneo la Menejimenti ya ujumuishwaji wa Anuai za Jamii ikiwemo udhibiti wa VVU, UKIMWI na MSY mahali pa kazi katika Utumishi wa Umma.

Aidha, Bw. Kapinga amewashukuru Viongozi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Wataalam wa afya kwa kushirikiana kuandaa kambi hiyo ambayo ni muhimu kwa watumishi wa umma kwani asilimia kubwa huathirika na magonjwa yasiyoambukiza pasipo wao kujua.

Pia amewapongeza waajiri wa Wizara na Taasisi zote ambao wameridhia watumishi wao kushiriki zoezi hilo muhimu kwani mwitikio umekuwa ni mkubwa.

Awali akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi ameishukuru Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuratibu na kusimamia kwa kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa katika zoezi la Kambi ya Uchunguzi, Ushauri na Elimu ya Afya kwa watumishi wa Umma katika Wizara, Taasisi na sekta binafsi.

Naye, Mkurugenzi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa Magufuli amewashukuru Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kukubali kushiriki zoezi hilo la Kambi ya Uchunguzi, Ushauri na Elimu ya Afya kwa watumishi wa Umma kwani mwitikio umekuwa mkubwa wa watumishi hao kutaka kujua hali zao za afya.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeshirikiana na Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa katika kuratibu zoezi hilo ikilenga kuwafikia watumishi wa umma ili waweze kufahamu hali zao za afya na kupata ushauri wa kitaalam kutoka kwa Madaktari Bingwa.