Habari
OFISI YA RAIS-UTUMISHI, BODI YA MIKOPO ZANZIBAR ZASAINI MAKUBALIANO KUBADILISHANA TAARIFA
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imesaini makubaliano ya ushirikiano na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Zanzibar (ZHELB) kwa ajili ya kuwezesha kubadilishana taarifa kati ya Mfumo wa Taarifa za Watumishi wa Umma wa Tanzania Bara na mfumo wa Bodi hiyo.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo, Agosti 12, 2026 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Zanzibar Ndugu Umrat Mohamed.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Katibu Mkuu Mkomi amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kutumia mifumo ya kidijitali kuboresha usimamizi wa taarifa na utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma.
Amesema kubadilishana taarifa hizo kutasaidia kubaini wanufaika wa mikopo ambao ni watumishi wa umma na kuwezesha wale wenye madeni ya mikopo kutekeleza wajibu wao wa kurejesha fedha walizogharamiwa na Serikali.
“Utaratibu huu utasaidia kuhakikisha taarifa za watumishi wanaonufaika na mikopo zinapatikana kwa usahihi na kwa wakati, jambo litakalorahisisha urejeshaji wa mikopo na kuimarisha usimamizi wa fedha za Serikali,” amesema Bw. Mkomi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Mwanakhamis A. Ameir, ameishukuru Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuwezesha hatua hiyo, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuimarisha mifumo ya taarifa na usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu Zanzibar.
Amesema kuunganishwa kwa mifumo hiyo kutarahisisha upatikanaji na uhakiki wa taarifa za wanufaika, hivyo kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mikopo na urejeshaji wake.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa Taasisi hizo katika usimamizi wa taarifa, kuongeza usahihi wa taarifa za wanufaika wa mikopo na kuwezesha huduma kutolewa kwa haraka, uwazi na ufanisi zaidi, sambamba na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utendaji wa Serikali.
Hatua hiyo pia inaweka msingi wa mifumo ya Serikali Mtandao kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa ufanisi, kwa kuzingatia taratibu za usalama na usiri wa taarifa.
