Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

NAIBU WAZIRI SANGU: TAKUKURU IJIPAMBANUE KWA KUTENDA HAKI NA UADILIFU


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa    (TAKUKURU) kuwa  mfano kwa kujipambanua kutenda haki na kuonesha  uadilifu katika jamii huku akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa  kwa Mtumishi yeyote wa TAKUKURU atakayebainika kuwa  sio muadilifu

 

Mhe. Sangu ametoa kauli  hiyo leo mara baada ya  kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora uliogharimu kiasi cha Sh. Milioni 314.2  hadi kukamilika kwake.

 

Amesema TAKUKURU ni chombo  kinachohitaji watumishi wenye uadilifu wa hali ya juu hivyo kwa Mtumishi yeyote  ambaye sio muadilifu TAKUKURU  si mahali sahihi kwa yeye kufanya kazi

 

Amesema ni jambo lisilokubalika kwa chombo hicho nyeti cha kuzuia rushwa halafu kukawa na Watumishi  mabingwa  wa kupokea. 

 

Akizungumzia ujenzi wa ofisi hizo, Mhe. Sangu ameipongeza TAKUKURU kwa kuonesha mfano namna fedha za Watanzania zinavyotakiwa kutumika  kwani  thamani ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi wa ofisi hizo unaonekana.

 

‘‘ TAKUKURU ni chombo kinachosimamia uadilifu na kinatakiwa kiwe cha kwanza kuonesha uadilifu kwa matendo yake, kwa  namna nilivyokagua jengo hili nimeridhishwa mno naamini wateja wetu watakaokuja hapa kwa ajili ya kuchunguzwa hili jengo litumike kama mfano kwa kuonesha thamani ya fedha iliyotumika, niwapongeze sana kwa jambo kubwa mlilolifanya hapa’’ amesisitiza Mhe. Sangu

 

Hata hivyo, Mhe. Sangu ameiagiza TAKUKURU kuhakikisha inahamia katika ofisi hizo za kisasa  ndani ya mwezi huu ikizingatiwa kuwa ofisi wanazozitumia kwa sasa katika Wilaya hiyo kodi yake ya  pango itafikia ukomo mwezi huu.

 

Amesema kukamilika kwa Ofisi hizo  kunaonesha dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha TAKUKURU inawajibika ipasavyo kwa wananchi.

 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Sangu ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake  makubwa ya kukubali kutoa fedha hizo ili kuhakikisha Watumishi wa  Takukuru  katika Wilaya ya Nzega wanatimiza  wajibu wao kwa kufanya kazi  katika Ofisi za  kisasa.

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu ameitaka TAKUKURU kuzifanyia kazi kwa wakati nyaraka za mikataba ya miradi ya maendeleo ambazo huwasilishwa kwao kutoka kwa  Wateja wao   

 

Amesema kama jambo limekamilika au halina uchunguzi wowote ni muhimu nyaraka hizo zikarudishwa haraka  kwa wahusika badala ya kukaa nazo kwa kipindi cha muda mrefu kwani lengo la  TAKUKURU kupewa nyaraka hizo ni kuzuia rushwa  ili  kuhakikisha miradi hiyo ya maendeleo inapoanza kutekelezwa isiharibike

 

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa nyaraka hizo za mikataba kufanyiwa kazi ipasanyo ili kuhakikisha  miradi hiyo ya maendeleo inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuonesha thamani ya fedha.