Habari
NAIBU WAZIRI SANGU: e-GA NI TAASISI NYETI KWA USALAMA WA TAIFA
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni Taasisi nyeti kwa ajili ya usalama wa nchi kwani kwani hakuna Mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) uliosanifiwa unaoweza kutumika nchini katika Wizara, Taasisi au Idara ya Serikali bila kuridhiwa na e-GA
Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria katika kikao cha Kamati hiyo na Watendaji wa e-GA na Taasisi ya Uongozi kilicholenga kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hizo ambapo amesema tangu kuanzishwa kwake e-GA imeleta mageuzi makubwa huku akitaja mifumo mingi inayotumika kwa sasa Serikalini imebuniwa na kusanifiwa na e-GA
Amesema ujio wa e-GA umeisaidia kupunguza gharama kubwa kwa Serikali ukilinganisha na hapo awali ambapo mifumo mingi iliyokuwa ikitumika kwenye Taasisi za Serikali ilikuwa ni ya kutoka nje huku akitolea mfano mfumo wa manunuzi wa TANEPS ulikuwa ukimlazimisha mtumiaji endapo kama anataka kufanya marekebisho ni lazima awasiliane na watengenezaji wa mfumo huo ambao ni Wagiriki
" Kama nchi kulikuwa hakuna usiri wa taarifa zetu, Wasanifishaji mifumo ya TEHAMA ambao ni wa kutoka Mataifa ya nje ndo walikuwa wenye ‘serve’ za taarifa zetu amesisitiza Mhe.Sangu
Amesema hapo awali Taasisi nyingi za Serikali zilikuwa zikitumia mifumo hiyo ya kutoka nje bila kuidhinishwa na e-GA ambapo ilikuwa ni rahisi kuhujumu kwa lengo la kujinufaisha kwa kushirikiana na watu wa kutoka nje ila kwa sasa hilo jambo haliwezekani kutokana na uwepo wa e-GA
'" Upo ushahidi kabisa kwamba e-GA imesaidia kuboresha utendaji kazi, imeimarisha utawala bora, kupunguza vitendo vya rushwa ambavyo vingeweza kujitokeza, kuimarisha makusanyo na kudhibiti matumizi ya maduhuli ya serikali” Mhe. Sangu amesisitiza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ameipongeza e-GA kwa kazi kubwa inayoendelea kuifanya huku akiitaka kjiimarisha zaidi kwenye eneo la ubunifu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia yanayotokea dunia kote
Hata hivyo Mwenyekiti huyo ameitaka e-GA kusanifu mifumo itakayosaidia kupunguza matatizo katika jamii ikiwemo upotevu mkubwa wa maji unaotokea katika maeneo mbalimbali nchini.