Habari
NAIBU WAZIRI SANGU AWANYOOSHEA KIDOLE WATUMISHI WA UMMA WAZEMBE, ASISITIZA WABADILIKE HARAKA
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema ajira ya kudumu Serikalini imekuwa ikisababisha watumishi wa umma kuwa wazembe na kukaa bila kufanya kazi wakiamini ikifika mwisho wa mwezi watapata mshahara jambo ambalo ni kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo Desemba 19, 2024 jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha siku tatu cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.
Amesema masharti ya ajira ya kudumu na mafao Serikalini kwa Watumishi wa Umma yanawaharibu watumishi ambapo wamejikuta wakifanya kazi kwa mazoea bila kuchukuliwa hatua licha ya kukiuka Sheria, Taratibu na Kanuni jambo ambalo linaweza kuisababishia serikali hasara kubwa.
Mhe. Sangu amesema katika ziara aliyoifanya kwenye baadhi ya mikoa amebaini changamoto hizo hasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo kuna baadhi ya maeneo amekuta Watendaji wa Kata na Vijiji wakifanya kazi kama miungu watu bila kuchukuliwa hatua za nidhamu licha ya kulewa asubuhi mpaka jioni huku wananchi wakikosa huduma.
"Nimefika moja ya eneo ambalo Mtendaji wa Kijiji na Kata analewa kuanzia asubuhi mpaka jioni siku zote za kazi, wananchi wanahitaji huduma hawapati, ukimuuliza mwajiri anasema ndio kawaida yake tumeshamzoea, katika utumishi wa umma hakuna mazoea ya namna hiyo na haikubaliki hata kidogo," alisema Mhe. Sangu.
Pia, alizitaja changamoto nyingine alizokutana nazo katika maeneo hayo kuwa ni uzembe , vitendo vya rushwa, ulevi uliokithiri, kutoa lugha zisizofaa, unyanyasaji, uonevu na ubinafsi hasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kutopandishwa vyeo, kutolipa malimbikizo ya mishahara, na suala la uhamisho.
Amesema, wamebaini kuwa changamoto zote hizo zimesababishwa na watumishi wazembe, wabinafsi na wasiotaka kuwajibika kwa weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizunguzia changamoto ya uhamisho, Naibu Waziri huyo amesema kuwa mtumishi anahamishwa zaidi ya mara sita ndani ya miaka saba, bila kulipwa madai yake ya uhamisho jambo ambalo linasababisha malimbikizo makubwa ya madai ambayo halmashauri husika haiwezi kuyalipa hivyo kuomba msaada Serikali Kuu na kuisababishia Serikali hasara kubwa.
"Unaweza kukuta madai yanafikia robo tatu ya mapato ya ndani ya halmashauri hivyo kusababisha ugumu wa kuyalipa, niwaase mtekeleze majukumu yenu kwa waledi, mtumishi anapohamishwa hakikisheni analipwa kwa wakati si kulimbikiza madai," amesistiza .
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (UTUMISHI), Bw. Juma Mkomi akizungumzia utekelezaji wa maagizo ya Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuhusu watumishi waliobainika kughushi barua amesema, tayari ameshachukua hatua na kuwaandikia barua waajiri wote kuzichunguza kwa siri barua zote wanazozipokea na kubaini kama ni halisi kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI.
Katibu Mkuu Mkomi amesema, zipo barua ambazo zinatengenezwa mtaani na kuwekewa nembo ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI, hivyo katika kukomesha vitendo hivyo visivyokuwa na maadili onyo kali linatolewa kwa wanaohusika na vitendo hivyo na hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Kikao kazi hicho kimewashirikisha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika na Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Kaulimbi ya kikao kazi hicho ni “Kusimamia Sera na Sheria za Utumishi wa Umma Kupitia Mifumo ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa Kidijitali Iliyoboreshwa.”