Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

NAIBU WAZIRI SANGU ATANGAZA MUUNDO MPYA WA UTUMISHI WA KADA YA UUGUZI NA UKUNGA KUANZA KUTUMIKA  MWAKA  FEDHA 2025/2026


 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu ametangaza kuanza  kutumika kwa Muundo  mpya  wa Utumishi wa Maendeleo ya kada za Uuguzi na Ukunga ifikapo  mwezi Julai  mwaka huu.

Amesema  utekelezaji wa muundo huo utasaidia kuongeza morali ya utendaji kazi kwa wataalamu wa Kada hiyo pamoja na kuboresha maslahi yao.

Amesema Serikali imesikia kilio cha Wauguzi hao  kilichodumu  kwa zaidi ya miaka 12 kutokana na muundo wa mwaka 2009 ambao unatumika hadi hivi sasa kuwa changamoto nyingi ikiwemo kutokutambua kada ya Wauguzi na Wakunga  wenye shahada ya juu na wenye shahada ya uzamili.

 

Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo  leo Ijumaa Aprili 10, 2025 Mkoani Iringa wakati akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,   Mhe. George Simbachawene kwenye ufunguzi wa   Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 54 wa Chama Cha Wauguzi Tanzania unaofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia leo kukiwa na jumla ya Washiriki  1500.

 

Amesema kutokana na changamoto za muundo huo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais. UTUMISHI na Utawala Bora , Baraza la Uuguzi na Ukunga na Vyama vya Kitaaluma ilipitia muundo huo na kurekebisha changamoto zilizokuwepo na hivi   sasa upo tayari kwa hatua za utekelezaji.

 

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imeamua kurekebisha muundo huo kwani muundo huo  umekuwa na mapungufu kwa  wataalamu wa kada hiyo.

 

Katika hatua nyingine  Mhe.Sangu ameziagiza Mamlaka za ajira nchini ifikapo  Mei 31, 2025 zihakikishe zinawasilisha orodha ya Watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo wakiwemo wauguzi na wakunga  huku akisisitiza  kuwa  bajeti ya kiasi cha Sh. Bil.207 zimeshatengwa kwa ajili ya upandishaji vyeo

 

Wakati huo huo, Mhe.Sangu amezitaka Mamlaka za Ajira  nchini kuhakikisha orodha ya Watumishi wakiwemo Wauguzi  wanaodai malimbikizo ya mishahara yawasilishwe  Ofisi ya Rais Utumishi ifikapo  Mei 31, 2025  yakiwa yamehakikiwa, ili baada Ofisi hiyo kujiridhisha yawasilishwe Hazina kwa ajili ya taratibu za malipo

 

Akizungumzia suala la uhaba wa  Watumishi wa Kada hiyo ya Wauguzi,  Mhe.Sangu amesema  Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha  Uongozi amewekeza vya kutosha kwenye sekta ya afya ikiwemo vifaa tiba na miundombinu ya afya. 

 

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Sangu amesema Rais  Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amekubali kutoa kibali cha ajira zipatazo 33, 212 na kati ya hizo takribani ajira  11,000   ni kwa ajili ya  kada ya afya ikiwemo wauguzi na wakunga   hali itakayochangia  kuongeza nguvu na  ufanisi kwa Watumishi wa kada hiyo katika utoaji huduma bora kwa wananchi

 

Awali, Rais wa Chama cha Wauguzi,  Bw. Alexander Baluhya amesema uwekezaji mkubwa umefanyika kwenye sekta ya afya  lakini  umekuwa hauendani na huduma zinazotolewa kutokana na uhaba wa Wauguzi na hivyo kupelekea wananchi kupata huduma zisizoridhisha.

 

Amesema hapo awali kulikuwa na vituo vichache  vya afya lakini kutokana na  uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan idadi ya vituo hivyo imeongezeka maradufu  hadi kufikia  vituo vipatavyo  1,038 na hivyo  kupelekea Wauguzi na Wakunga  kuwa na majukumu mengi kupita uwezo wao.

 

Bw.Baluhya amesema suala la  upandishaji   madaraja kwa Wauguzi imekuwa changamoto kubwa licha ya Wauguzi hao kuwa sifa stahiki za kuweza kupanda vyeo.

 

Amesema hali hiyo imekuwa ikiwaathiri na kushusha morali kwa Wauguzi hao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

 

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe.Peter Serukamba amewataka Wauguzi hao kufanya kazi kwa weledi  huku akiwasisitiza umuhimu wa kujiendeleza ili kujitafutia maarifa mapya kutokana na mabadiliko makubwa ya teknolojia yanayotokea duniani kote.

 

Amesema Serikali ya Awamu ya  Sita imejenga  vituo vya Afya na Zahanati kila kona ya nchi hivyo hilo haliwezi kutimia kama Wauguzi watakuwa hawana maarifa mapya pamoja na kuwa na lugha mbaya pindi wanapowahudumia wagonjwa.

 

Hata hivyo Mhe.Serukamba  ametumia fursa hiyo kuzitaka Halmashauri za Wilaya nchini kutimiza  wajibu wao kwa kuhakikisha Wauguzi wanapandishwa madaraja yao pamoja na kulipwa stahiki zao pindi wanapokwenda  likizo." Tusiwabebeshe mzigo w Ofisi ya Rais  Utumishi na Utawala Bora haya mengine yapo chini ya uwezo wa  Halmashauri zetu " amesisitiza