Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

NAIBU WAZIRI SANGU APONGEZA WIZARA NA TAASISI ZA UMMA KWA KUWA NA UTAYARI WA KUWAHUDUMIA WATUMISHI WA UMMA NA WANANCHI KATIKA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ametoa pongezi kwa Wizara na Taasisi za Umma kwa kuwa na utayari wa kuwahudumia watumishi wa umma na wananchi katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

“Tumekuwa tukifanya kliniki katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili Watumishi wa Umma na Wananchi, lakini kupitia Maadhimisho haya ya Wiki ya Utumishi wa Umma yamekuwa suluhisho kwa kufanya kazi papo kwa hapo kwani  Watumishi wa Umma na Wananchi wamekuja kuhudumiwa kwa wakati,hii inaonesha ni kwa namna gani mmekuwa na utayari wa kutoa huduma bora kwa maslahi ya taifa, hongereni sana,” Mhe. Sangu amesema

Aidha, Mhe. Sangu ametoa rai kwa Watanzania wote kufika katika Viwanja hivyo ili kupata huduma za moja kwa moja na elimu kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara na taasisi za Umma.

Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali watumishi wa umma nchini kwa kuboresha maeneo yao ya kazi kwa kuwa sehemu salama ili watanzania waweze kupata huduma bora.