Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

NAIBU WAZIRI QWARAY ATOA WITO KWA WATUMISHI WA UMMA KUTUMIA MFUNGO WA MWEZI WA RAMADHANI NA KWARESMA KUJITAFAKARI JUU YA HUDUMA WANAZOZITOA KWA WANANCHI


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray ametoa wito kwa Watumishi wa Umma nchini kutumia kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Mafungo ya Kwaresma kujitafakari juu ya namna wanavyotoa huduma kwa wananchi.

Naibu Waziri Qwaray ametoa wito huo wakati wa futari maalum iliyoandaliwa na Menejimenti ya Ofisi hiyo katika kipindi hiki ambapo Watumishi wa imani ya Dini ya Kiislam na Kikristo wanakuwa katika mfungo.

Mhe. Qwaray amesema watumishi wa umma wanatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, huruma na unyenyekevu huku wakimtanguliza Mungu hivyo ni vema wakajitafakari  kama hayo yote yanafanyika. 

Ameongeza kuwa, kipindi cha mfungo kisiwe cha kushinda njaa bali iwepo thawabu kwa Mungu ambayo itatokana na huduma bora zitakazotolewa na watumishi hao kwa wananchi itakayoleta matokeo chanya kwa ustawi wa nchi.

Aidha, amepongeza Menejimenti ya Ofisi hiyo kwa kuwakumbuka wahitaji ambao walijumuika nao katika futari hiyo maalum iliyokutanisha makundi ya watu tofauti ambayo yanasaidia kubadilishana uzoefu ili kuboresha utendakji kazi hasa katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesisitiza kuendelea kuiombea nchi na viongozi. “Niwasisitize tuendelee kuiombea nchi yetu na tuitunze amani tuliyonayo, sisi sote ni wamoja na ni Watanzania hatuulizani dini wala kabila,alisisitiza Mhe. Qwaray.

Awali Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Juma Mkomi alisema futari hiyo iliandaliwa kwa lengo la kuwaweka pamoja watu wa makundi mbalimbali hasa katika Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani na Kwaresma.

Bw. Mkomi aliongeza kuwa ni fursa nzuri kukutana kwa wakati mmoja kwani ibada hizo huwafanya kuwa wacha Mungu jambo ambalo husaidia watumishi kuwa na maadili ya kuwatendea haki wananchi wanaowahudumia.