Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

NAIBU WAZIRI MHE. QWARAY AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUZUIA UDANGANYIFU


Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amewataka watumishi wa umma kushiriki kikamilifu katika kuzuia udanganyifu na kulinda rasilimali za umma, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na wataalamu wa udhibiti wa vitendo hivyo.

Mhe. Qwaray ameyasema hayo leo, Novemba 16, 2026, jijini Arusha, wakati akifungua mkutano na kongamano la mwaka la Taasisi ya Wataalamu wa Udhibiti wa Udanganyifu Tanzania (ACFE).

Amesema mapambano dhidi ya udanganyifu hayapaswi kuachiwa wakaguzi pekee, bali kila mtumishi wa umma ana wajibu wa kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya utumishi.

“Kila mtumishi wa umma ni mlinzi wa rasilimali za umma. Hivyo, jukumu la kuzuia udanganyifu si la wakaguzi pekee, bali ni la kila mtumishi kwa kuzingatia nafasi, mamlaka na wajibu wake katika taasisi,” amesema Mhe. Qwaray.

Amesisitiza umuhimu wa maafisa utumishi, maafisa rasilimali watu na vyama vya kitaaluma kushirikiana na ACFE Tanzania katika kuwajengea uwezo watumishi wa kubaini viashiria vya udanganyifu na kuimarisha maadili mahali pa kazi.

Mhe. Qwaray amesema utaalamu wa ACFE unaweza kusaidia kuimarisha mifumo ya upimaji wa utendaji kazi na kuzuia upotoshaji wa takwimu, ili taarifa zinazowasilishwa na taasisi za umma ziakisi matokeo halisi ya utekelezaji wa majukumu.

Katika hatua nyingine, ameikaribisha ACFE kuwasilisha mapendekezo ya kitaalamu kwa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kuhusu maeneo yanayoweza kujengewa ushirikiano katika kuimarisha utendaji kazi, nidhamu na maadili ya watumishi wa umma.

Akizungumzia maendeleo ya teknolojia, Mhe. Qwaray amesema matumizi ya akili mnemba na fedha za kidijitali yameibua vihatarishi vipya vya udanganyifu vinavyohitaji mbinu za kisasa za udhibiti.

“Teknolojia haiwezi kuchukua nafasi ya uadilifu wa binadamu,” amesema. Pia, amesisitiza umuhimu wa kujenga mazingira salama kwa watumishi na wananchi kutoa taarifa kuhusu udanganyifu bila hofu ya vitisho au kulipiziwa kisasi.

Naye Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhandisi Keneth Nindie amesema wizara hiyo imeunda mifumo mbalimbali ya kubaini vihatarishi vya udanganyifu na inaendelea kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani ili kuzuia vitendo hivyo kabla ya madhara kutokea.

Amesema ili mifumo hiyo iwe na tija, ni muhimu taasisi mbalimbali kuhakikisha zinaitumia ipasavyo.

Kwa upande wake, Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya ACFE Tanzania, Bw. Ali Mabrouk Juma amesema kuwa na bajeti kubwa na watumishi wa kutosha hakutoshi iwapo taasisi haina mikakati madhubuti ya kupambana na udanganyifu.

Amesema kasi ya maendeleo ya teknolojia inahitaji taasisi kuhuisha mbinu za udhibiti na kuwajengea uwezo watumishi kutumia mifumo ya kisasa kubaini udanganyifu.

Bw. Juma amesema ACFE haikusudii kuchukua majukumu ya taasisi nyingine, bali kuongeza nguvu katika juhudi za kupambana na udanganyifu.

Aidha, ameiomba Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutambua kada ya wataalamu wa udhibiti wa udanganyifu, huku akimwomba Qwaray kuwa mlezi wa taasisi hiyo.

Kongamano hilo linafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), likijikita katika mikakati ya kudhibiti udanganyifu katika zama za akili mnemba, takwimu na fedha za kidijitali.