Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

NAIBU WAZIRI MHE. QWARAY ATAKA WATUMISHI KUZINGATIA MAADILI KUFANIKISHA DIRA 2050


Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, amewataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili, weledi, uwajibikaji na usikivu ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuleta ustawi wa wananchi.

 

Amesema katika mwaka huu wa fedha, Ofisi ya Rais – Utumishi imepanga kuanza zoezi la ujumuishaji wa programu za maadili katika taasisi za umma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kujenga Utumishi wa Umma wenye watumishi waadilifu.

 

Mhe. Qwaray ametoa kauli hiyo leo, Novemba 26, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha saba cha kubadilishana uzoefu baina ya Ofisi ya Rais – Utumishi, taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma.

 

“Katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, watumishi wa umma wenye uadilifu ni nguzo muhimu ya kufanikisha maono ya Taifa na kuleta ustawi wa wananchi,” amesema Mhe. Qwaray.

 

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kujenga Utumishi wa Umma unaozingatia maadili, weledi, uwajibikaji na usikivu.

 

Hata hivyo, Mhe. Qwaray amesema licha ya jitihada za Serikali kuimarisha mifumo ya kidijitali ya usimamizi, udhibiti na utoaji wa huduma, bado taarifa za viashiria vya ukiukwaji wa maadili zinaendelea kujitokeza.

 

Ametaja baadhi ya vitendo hivyo kuwa ni rushwa, uvujishaji wa siri za Serikali, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, hujuma dhidi ya miradi ya maendeleo, upendeleo, matumizi ya lugha zisizo na staha na kukosekana kwa uzalendo.

 

Amesema hali hiyo inahitaji wadau kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kutafuta mbinu madhubuti za kuzuia na kushughulikia ukiukwaji wa maadili.

 

Mhe. Qwaray amezitaka taasisi kuweka mazingira rafiki ya kupokea na kushughulikia mrejesho wa wananchi, kuhakikisha miongozo ya maadili inapatikana kupitia tovuti rasmi za taasisi na viongozi kuwa mfano wa kuigwa.

 

“Watumishi hujifunza si kwa maelekezo pekee, bali pia kwa kuangalia vitendo, mienendo na maamuzi ya viongozi wao,” amesema Mhe. Qwaray.

 

Pia, amezitaka taasisi kuwajengea uwezo watumishi kuhusu maadili, kuhakikisha kila mtumishi anapata nakala ya kielektroniki ya Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma na kusimamia matumizi sahihi ya Hati ya Ahadi ya Uadilifu.

 

Mhe. Qwaray amesisitiza matumizi ya Serikali Mtandao, kuhakikisha kila mtumishi ana anuani rasmi ya barua pepe ya kikazi na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kubaini hali ya uadilifu katika taasisi.

 

Aidha, amezipongeza taasisi simamizi za maadili kwa kuendelea kusimamia tabia na mienendo ya watumishi na kutumia vikao hivyo kuboresha mbinu za usimamizi wa maadili.

 

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Utumishi, Bi. Leila Mavika, amesema vikao hivyo ni sehemu ya jitihada endelevu za kubadilishana uzoefu katika kujenga Utumishi wa Umma wenye maadili na uwajibikaji ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

 

Amesisitiza kuwa vikao hivyo ni muhimu katika kuwakumbusha watumishi wajibu wao wa kutoa huduma bora kwa wananchi bila upendeleo na bila kuwalazimisha kutoa rushwa ili kupata huduma.