Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

NAIBU WAZIRI KIKWETE ; MATUMIZI YA MFUMO WA USAILI WA KIDIGITALI UNAKUZA UWAZI KWENYE MCHAKATO WA KUTOA AJIRA SERIKALINI


 

Na. Lusungu Helela-Dar es Salaam

 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete  amesema kitendo cha Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuanza kutumia rasmi mfumo wa usaili wa kidigitali unaomuwezesha mwombaji  kusailiwa  eneo alilopo badala ya kusafiri  umbali mrefu, ili kupunguza gharama  kwa Serikali na kwa wanaosailiwa ni mafanikio makubwa ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwazi kwenye mchakato wa kutoa ajira.

 

Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo jana Jijini  Dar es Salaam  mara baada ya  kushuhudia  wasailiwa wa kada ya Tehama wakifanya usaili huo katika  Chuo Kikuu cha St. Joseph , ikiwa ni moja ya kituo cha usaili  wa mchujo unaofanyika  kidigitali  katika kila Mkoa Nchi nzima, ikiwa ni usaili wa kwanza tangu mfumo huo ulipozinduliwa hivi karibuni

 

Amesema mfumo huo umeanza kutumika wakati sahihi ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea na jitihada za kuimarisha uwazi na kuepuka upendeleo katika suala zima la utoaji ajira serikalini.

Amesema vituo vipatavyo 32 nchi nzima leo vimeendesha usaili huo ambapo  jumla ya wasailiwa 2325 wamepata fursa ya kufanya usaili huo pasipo kulazimika  kusafiri umbali mrefu

 

Amefafanua kuwa vituo 32 kulikofanyika usaili huo kunajumuisha Tanzania Bara na Visiwani ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam kulikuwa na vituo vinne kutokana na idadi kubwa ya wasailiwa waliokuwa wameomba .

 

 

 

 

 

 

Mhe.Kikwete amesema  suala la ajira ni maisha ya watu, hivyo  mchakato huo leo umefungua ukurasa mpya   wa kukuza  uwazi  na uadilifu katika  kuondoa  manung'uniko  kwa wale  ambao wanatafuta ajira serikalini.

 

Amesema mfumo huo mbali ya kusaidia kupunguza gharama  za wasailiwa  ambao  walikuwa wanalalamika kusafiri  umbali mrefu kwenda  kwenye  kituo cha usaili kwa kutumia muda mwingi  na gharama kubwa, ila  leo hii wamesailiwa  mahali walipo  na kisha  kuendelea kufanya shughuli zingine za kujiingizia kipato.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Tehama kutoka Sekretariet ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Mhandisi Samweli Tanguye  amesema  mfumo huo mara baada ya wasailiwa hao kumaliza kufanya mchujo watapata matokeo yao leo tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo matokeo hayo yalikuwa yakichukua zaidi ya siku tatu kutoka.

 

Amesema mfumo huu unatoa nafasi kwa Wasailiwa ambao wanafanya usaili zaidi ya mmoja ndani ya siku moja kuwa wigo wa kufanya usaili mwingine siku hiyo hiyo kwa saa tofauti ambapo awali haikuwa rahisi.

 

Kwa upande wake Juma Ali, Msailiwa wa kada ya Tehama amepongeza ujio wa mfumo huo wa usaili wa kidijitali huku akisema licha ya kumpunguzia gharama ya kusafiri hadi Jijini Dodoma lakini  amepata fursa ya kuendelea kufanya shughuli zingine mara baada ya kumaliza usaili wake