Habari
NAIBU KATIBU MKUU UTUMISHI NA UTAWALA BORA BW. DAUDI AKUTANA NA WADAU WA TAASISI ZA ELIMU YA JUU KUWEZESHA UTEKELEZAJI WA MABORESHA YA MFUMO WA e-UTENDAJI YALIYOFANYIKA

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Washiriki kutoka Taasisi za Elimu ya Jùu kushiriki kikamilifu katika Kikao cha Kazi cha kuwezesha utekelezaji wa maboresho ya mfumo wa e-Utendaji kwa ajili ya kutumika katika Taasisi za Elimu nchini.
Hatua hiyo inakuja kufuatia Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora kutambua tofauti za mifumo ya kiuendeshaji iliyopo katika Taasisi za Elimu ya Juu na Taasisi nyingine za Umma.
Bw. Daudi ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma kwenye Kikao cha Kazi cha kuwezesha utekelezaji wa maboresho ya mfumo wa e-Utendaji utakaokuwa ukitumika katika Taasisi za Elimu ya Juu ambapo katika kikao kazi hicho jumla ya Taasisi 25 zimeshiriki.
Akizungumzia matumizi ya mfumo huo, Bw. Daudi amesema mwaka 2023/24 Serikali ilianza utekelezaji wa mfumo wa e-Utendaji katika Taasisi za Umma lakini hata hivyo kwa nyakati tofauti Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekua ikipokea mrejesho na changamoto katika utekelezaji wake katika Taasisi za Elimu ya Juu.
Kutokana na hilo, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora ilikuwa ikipokea maoni ya kuboresha mfumo wa e-Utendaji ili kuwezesha mfumo husika kutekelezwa kwa ufanisi katika Taasisi za Elimu ya Juu.
Naibu Katibu Mkuu Bw. Xavier Daudi amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imejipanga kuhakikisha inaboresha utekelezaji wa Mfumo huo katika Taasisi za Umma kulingana na uhalisia na mazingira ya Taasisi husika.
Kufuatia hatua hiyo, Ofisi ilipokea na kufanyia kazi maoni ya kuboresha Mfumo wa e-Utendaji na maboresho kwa Taasisi za Elimu ya Juu kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.
Bw. Daudi amewataka Washiriki hao kuhakikisha maboresho yaliyofanyika katika mfumo wa e-Utendaji na matokeo yanayotarajiwa yanafika katika ngazi ya mtumishi na taasisi kwa ujumla.