Habari
NAIBU KATIBU MKUU LWANGILI ASISITIZA UZINGATIAJI WA SHERIA KATIKA USHUGHULIKIAJI WA MASHAURI YA NIDHAMU KATIKA UTUMISHI WA UMMA
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni katika kushughulikia mashauri ya nidhamu katika Utumishi wa Umma, akieleza kuwa uzingatiaji wa misingi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka.
Bi. Lwangili ameyasema hayo leo, tarehe 31 Agosti, 2026, wakati akihitimisha mafunzo yaliyolenga kuwajengea Watumishi wa Ofisi ya Rais–UTUMISHI uelewa kuhusu Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma, yaliyofanyika katika eneo maalumu la Ofisi hiyo, Mtumba, jijini Dodoma.
Bi. Lwangili amesema katika kushughulikia masuala ya nidhamu ni muhimu kuhakikisha kuwa thamani na utu wa mtu vinalindwa, huku hatua zote zikichukuliwa kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa katika kushughulikia mashauri ya nidhamu, Sheria, Taratibu na Kanuni zinafuatwa ili haki itendeke, huku tukilinda thamani na utu wa mtu, amesema Bi. Lwangili.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwakumbusha Watumishi wa Umma kuhusu madhara ya kutokuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni katika utekelezaji wa majukumu yao, akieleza kuwa uelewa huo utasaidia kupunguza makosa na kuwaepusha watumishi na changamoto ya kufikishwa katika mashauri ya nidhamu.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye ni Afisa Sheria Mwandamizi, kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Edwin Bilikundi, amesema usimamizi wa nidhamu katika Utumishi wa Umma umejengwa katika dhana mbili kuu ambazo ni kurekebisha mwenendo wa Mtumishi (corrective measures) na utoaji wa adhabu (sanction approach). Amesema njia ya kurekebisha inalenga kumsaidia Mtumishi kutambua kosa na kujirekebisha, wakati utoaji wa adhabu hutumika pale kosa linapothibitika, hususan kwa makosa yanayojirudia au yenye uzito.
Bw. Bilikundi ameongeza kuwa mchakato wa nidhamu unapaswa kuanza kwa uchunguzi wa awali unaolenga kubaini ukweli na uzito wa tuhuma, pamoja na kuamua hatua stahiki za kuchukua.
Amesisitiza kuwa uzingatiaji wa hatua na muda uliowekwa katika Sheria, Kanuni na Taratibu ni muhimu katika kuhakikisha mchakato wa nidhamu unakuwa wa haki na wenye msingi sahihi wa kisheria.
