Habari
NAIBU KATIBU MKUU LWANGILI ASISITIZA UJUZI NA HAIBA YA UONGOZI KATIKA URITHISHANAJI MADARAKA KWA WATUMISHI WA UMMA
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kujenga ujuzi wa kitaalamu na haiba ya uongozi katika kuwaandaa warithi wa madaraka ili kuhakikisha kunakuwa na mwendelezo wa utendaji na utoaji wa huduma bora katika Taasisi za umma.
Bi. Lwangili ameyasema hayo leo, Agosti 10, 2026, wakati akihitimsha mafunzo ya uelewa kuhusu Urithishanaji Madaraka yaliyofanyika katika eneo maalumu la Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Mtumba Jijini Dodoma.
Amesema maandalizi ya urithishanaji madaraka yanapaswa kuanza mapema kwa kuwajengea uwezo unaohitajika katika nafasi za uongozi wanazotarajiwa kuzishika.
Aidha, Bi. Lwangili ameongeza kuwa ujuzi wa kitaalamu (Technical Skills) humwezesha Mtumishi kuwa na maarifa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku haiba ya uongozi ikimsaidia kuwasiliana vizuri, kujiamini, kushirikiana na wengine, kuwa mwadilifu, kufanya maamuzi na kuwajibika.
“Kuwa na ujuzi wa kitaalamu pekee hakutoshi. Mtumishi anayejengwa kuwa Kiongozi wa baadaye anapaswa pia kuwa na haiba inayomjengea uwezo wa kuwasiliana vizuri, kujiamini, kushirikiana na wengine, kuwa mwadilifu, kufanya maamuzi na kubeba majukumu kwa uwajibikaji,” amesema Bi. Lwangili.
Pia Bi. Lwangili amesisitiza kuwa, Urithishanaji Madaraka si kumwandaa mtu kuchukua nafasi ya Kiongozi aliyepo pekee, bali ni kuimarisha Taasisi kwa kuwa na Watumishi wenye uwezo wa kuendeleza majukumu na huduma za umma.
Kwa upande wake, Mchumi Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Bertha Bomani, ameeleza kuwa Urithishanaji Madaraka ni mchakato wa kuwaandaa mapema Watumishi wenye uwezo na sifa stahiki kwa ajili ya majukumu ya uongozi.
Bi. Bomani amebainisha mikakati ya Urithishanaji Madaraka katika Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya uelewa na kujenga uwezo kwa Viongozi na Watumishi kuhusu manufaa ya kuandaa na kutekeleza Mpango wa Urithishanaji Madaraka, pamoja na kuwakumbusha Waajiri kutenga fedha katika bajeti za Taasisi zao kwa ajili ya uandaaji na utekelezaji wa mpango huo.
