Habari
Mtumishi hodari wa mwaka 2025 wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Charles Shija (wa kwanza kulia aliyekaa) akifuatilia uhesabuji wa kura wakati wa kikao kazi cha kumchagua mfanyakazi hodari kilichofanyika katika eneo la ofisi hiyo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewasisitiza watumishi wa ofisi hiyo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi ili kuchochea maendeleo katika kuwahudumia wananchi.
Bw. Daudi ameyasema hayo leo wakati wa kikao kazi kilicholenga kumchagua mfanyakazi hodari wa mwaka 2025 wa ofisi hiyo kilichofanyika Mtumba jijini Dodoma.
Bw. Daudi amewataka watumishi wa ofisi hiyo kutoa huduma bora kwa kuzingatia Taratibu, Kanuni na Sheria za Utumishi wa Umma ili kujenga imani kwa Watumishi wa Umma na Wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya utoaji wa huduma bora kwa umma.
“Ushirikiano ni moja ya nguzo muhimu za ofisi yetu, hivyo endeleeni kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya kila siku, mfanyakazi hodari aliyepatikana anatokana na ushirikiano mzuri alioupata kutoka kwa watumishi wenzake wa ofisi hiyo”alisisitiza Bw. Daudi.
Bw. Daudi ameongeza kuwa, watumishi wote wa Ofisi hiyo ni wafanyakazi hodari ingawa mshindi ni lazima apatikane hivyo, amewataka watumishi wote kutokata tamaa kwani kila mmoja anawajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo.
Kikao kazi hicho kimemchagua Bw. Charles Shija kuwa mfanyakazi hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2025, mshindi wa pili ni Bw. Erick Andrea na washindi wa nafasi ya tatu ni watumishi wawili ambao ni Bw. Jumbe Mgoha na Bw. Waziri Mkumbo.