Habari
MRADI WA UJENZI WA MAKAZI YA WATUMISHI WA UMMA SEKTA YA ELIMU NA AFYA KUONGEZA TIJA KATIKA UTENDAJI KAZI
Timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Fedha na Watumishi Housing Investments ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Patrick Allute imefanya ziara ya kikazi iliyolenga kukagua na kufanya tathmini ya mwisho ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma wa Shule ya Sekondari Maluga yanayojengwa katika Kijiji cha Maluga, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba na Zahanati ya Makunda, Kijiji cha Makunda Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida ambapo kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza tija Serikalini.
Akizungumza kwa niaba ya timu hiyo mara baada ya kukagua mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Allute amesema, makazi ya watumishi wa umma yanapokuwa karibu na maeneo ya kazi huongeza ufanisi na uwajibikaji hivyo, utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya kwanza katika mikoa ya Dodoma, Singida, Lindi, Pwani na Ruvuma utamkomboa mtumishi wa umma katika utendaji kazi.
“Maeneo ya pembezoni yamekuwa na changamoto ya makazi na kusababisha baadhi ya watumishi wa umma kutokutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kupitia mradi huu unaotekelezwa kwa awamu ya kwanza katika mikoa ya Dodoma, Singida, Lindi, Pwani na Ruvuma unatarajiwa kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma kwenye maeneo hayo,” amesema Mkurugenzi Allute
Naye, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Mipango na Bajeti, Bi. Julieth Magambo amesema ili makazi hayo yawe na ubora wa kudumu ni vema Watumishi watakaoishi katika makazi hayo wakazingatia utunzaji wa miundombinu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji kutoka Watumishi Housing Investments, Bw. Paskali Massawe, amesema makazi hayo yamejengwa kwa kuzingatia ubora ili kuendana na malengo ya Serikali katika kuwatengenezea mazingira bora watumishi wa umma.
Kadhalika, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya fedha, Bw. Ezekiel Odipo ameeleza kuwa, ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuongeza tija kwa watumishi wa umma fedha nyingi imetolewa kwa lengo la kuboresha makazi ya watumishi hao ili waweze kutoa huduma bora kwa ustawi wa taifa.
