Habari
MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI WALETA MAPINDUZI MAKUBWA YA TEHAMA NCHINI IKIWEMO KURAHISISHA UTOAJI HUDUMA KWA WANANCHI NA WATUMISHI WA UMMA

Mradi wa Tanzania ya Kidijitali umeleta mapinduzi makubwa ya miundombinu ya TEHAMA nchini ikiwemo kuunganisha jumla ya taasisi za umma 600 ambazo ni Wizara, Mikoa, Halmashauri na Taasisi zote zilizohamia Dodoma ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na watumishi wa umma.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango wakati wa kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
“Mradi huu umeleta mafanikio makubwa katika kuunganisha Serikali kwenye mitandao ya TEHAMA ambapo taasisi 600 ikiwemo Wizara, Mikoa, Halmashauri na Taasisi zote zilizohamia Dodoma zimeunganishwa na mifumo ya TEHAMA ili kutoa huduma kwa wananchi na watumishi wa umma nchini,’’ amesema Bw. Kiwango
Ameongeza kuwa katika kutoa huduma bora, watumishi wa umma wameendelea kutekeleza majukumu yao kupitia mifumo mbalimbali na kupimwa kupitia mifumo iliyojengwa ya Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma na Taasisi (e-Utendaji).
Aidha, Mfumo wa Daftari la Huduma za Serikali utawasaidia wananchi kupata huduma sehemu moja kwa urahisi, kwa wakati na kwa uwazi.
Mkurugenzi Kiwango ametoa wito kwa wananchi kutumia simu zao za viganjani kupiga namba *152*00# kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za Serikali bila kufika katika ofisi husika endapo hawatakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.