Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MKOMI APONGEZA USHIRIKI TAASISI, WIZARA NA WADAU WIKI YA UTUMISHI WA UMMA


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Mkomi ametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza leo katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

 

Katika ziara hiyo, Bw. Mkomi alipata fursa ya kutembelea na kujionea huduma pamoja na mafanikio yanayowasilishwa na Wizara, Taasisi za Umma na wadau mbalimbali wanaoshiriki maadhimisho hayo, yenye lengo la kuhamasisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kuonesha mchango wa sekta ya umma katika maendeleo ya Taifa.

 

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda hayo, Bw. Mkomi amewapongeza washiriki wote kwa kujitokeza kwa wingi na kutumia maonesho hayo kuelimisha wananchi kuhusu huduma wanazozitoa pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana katika taasisi zao.

 

“Ninazipongeza Wizara, Taasisi na wadau wote walioshiriki maadhimisho haya kwa namna walivyoandaa mabanda yao na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi. Ushiriki huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” amesema Bw. Mkomi.

 

Aidha, amehimiza taasisi za umma kuendelea kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kusikiliza maoni ya wananchi na kuboresha huduma zinazotolewa ili ziendane na mahitaji ya wananchi na matarajio ya Serikali.

 

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa 2026 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘’Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu’’.