Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MKANDARASI SUMA JKT AHIMIZWA KUKAMILISHA JENGO LA eGA KWA MUJIBU WA MKATABA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amemtaka Mkandarasi SUMA JKT anayejenga ofisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kukamilisha haraka ujenzi wa jengo la ofisi hiyo kwa mujibu wa mkataba kwa kuwa  eGA ni kiini cha uendeshaji wa Serikali katika kujenga mifumo imara itakayoboresha utoaji wa huduma Serikalini.

Mhe. Simbachawene amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi hiyo jijini Dodoma.

“eGA ni kiini cha uendeshaji wa Serikali mtandao hivyo, tuna wajibu wa kurahisisha utendaji kazi wa taasisi za Serikali kwa lengo la kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi, hivyo tumieni nguvu nyingi kukamilisha ujenzi huu kwa mujibu wa mkataba na kwa wakati,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema, Serikali ya Awamu ya Sita kipaumbele chake kikubwa ni kuwa na Serikali ya Kidijitali ili kutoa huduma bora na kwa wakati, hivyo kukamilika kwa jengo hilo kwa wakati kutaisaidia Serikali kufikia malengo yake ya kujenga mifumo imara itakayoboresha utoaji wa huduma Serikalini.