Habari
MHESHIMIWA KIKWETE AONGOZA MAPOKEZI YA NAIBU KATIBU MKUU, OFISI YA RAIS – UTUMISHI BI. PRISCA LWANGILI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameongoza mapokezi ya Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bi. Prisca Lwangili aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan baada ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Xavier Daudi kustaafu Utumishi wa Umma.
Bi. Prisca Lwangili, amepokelewa rasmi leo na Viongozi na Watumishi wa ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mheshimiwa Kikwete amemkaribisha Bi. Lwangili na kumsihi kutumia uzoefu wake katika kazi kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo ili kuongeza uwajibikaji katika kuhudumia wananchi kwa ustawi wa Taifa
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mheshimiwa Regina Qwaray, amemkaribisha Bi. Lwangili na kueleza kuwa Viongozi pamoja na Watumishi wa Ofisi hiyo wapo tayari kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake mapya, ili kuimarisha utendaji wa ofisi kwa manufaa ya umma.
Naye Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Juma Mkomi, amesema uongozi na watumishi wa Ofisi hiyo wako tayari kushirikiana kwa karibu na Naibu Katibu Mkuu huyo ili kuhakikisha majukumu ya Ofisi yanatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
Kwa upande wake, Bi. Lwangili amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua katika nafasi hiyo ambapo ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa kujituma na kuongeza ubunifu ili kuhakikisha malengo ya ofisi hiyo yanafikiwa kwa manufaa ya Serikali na wananchi.
Aidha, ameishukuru ofisi hiyo kwa mapokezi aliyopata na kuahidi kufanya kazi kwa ufanisi katika kuwahudumia Wananchi.
