Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. SIMBACHAWENE AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUJIEPUSHA NA UHAMISHO USIOZINGATIA TARATIBU


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amewataka watumishi wa umma nchini kujiepusha na uhamisho usiozingatia taratibu za kiutumishi kwa kuwa ni kinyume cha maadili na adhabu yake ni kufukuzwa kazi.

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa Mkoa wa Geita wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinawazokabili watumishi hao katika utekelezaji wa majukumu yao.


“Tumegundua kwamba kuna baadhi ya watumishi wanafanya uhamisho feki, wala sio wa Katibu Mkuu-UTUMISHI wala TAMISEMI, tumeanza kuwafuatilia na kuwakamata na tutaendelea kuwakamata kwa sababu ni watumishi wa umma na hawana pakukimbilia,” amesema Mhe. Simbachawene.

Waziri Simbachawene ameongeza kuwa, watumishi hao waliokiuka taratibu za uhamisho wanaweza kufanikiwa kudanganya mambo mengine yote na kwenda kwenye vituo hivyo vya kazi wanavyovitaka lakini hawatofanikiwa kuhamisha mshahara kutokana na udhibiti wa mifumo iliyopo.

“Utahamisha kila kitu lakini kinachokuja kusumbua ni kuhamisha mshahara kwa kuwa huwezi kuuona, kwani Mhe. Rais ameuficha, hakuna udanganyifu kwenye eneo hilo,” amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Amewataka watumishi wote walioghushi uhamisho kurejea katika vituo vyao vya kazi vya awali vinginevyo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa ikiwemo kufukuzwa kazi.

Mhe. Simbachawene ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Geita yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani humo na kusikiliza changamoto za kiutumishi zinazowakabili ili kuzitatua.