Habari
MHE. SIMBACHAWENE AWATAKA WAAJIRI KUTENGA BAJETI YA WATUMISHI WA UMMA KUSHIRIKI SHIMIWI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amewataka Waajiri kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuwawezesha Watumishi wa Umma kushiriki Michezo ya SHIMIWI ili kukidhi malengo na misingi ya kuanzishwa kwa michezo hiyo ili kuleta tija iliyokusudiwa
Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Oktoba 5, 2024 Mkoani Morogoro wakati akifunga Mashindano ya 38 ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali Tanzania ( SHIMIWI) ambapo amesema michezo hiyo sio hiari bali ni lazima kwa Watumishi wa Umma nchini
Ametumia fursa hiyo kuwataka Makatibu Wakuu pamoja na Makatibu Tawala kuacha kudharau michezo hiyo huku akisisitiza kuwa michezo hiyo ipo kisheria.
Amesema michezo hiyo ni muhimu mbali ya kuimarisha afya kwa watumishi wa umma pia inawasaidia watumishi hao kuondoa msongo wa mawazo.
Kufuatia hatua hiyo Mhe, Simbachawene amewataka Watumishi hao walioshiriki michezo hiyo wakaoneshe utofauti mahali pa kazi ili kuendelea kuipa heshima michezo hiyo ili kuendelea kuwashawishi waajiri wao kutenga bajeti ya ushiriki
Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene amewataka Watumishi hao kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo amesema ushiriki wao ni muhimu sana kwa ajili ya mustakabali wa taifa endelevu.
‘’Watumishi walio wengi wanaona kujiandikisha na kushiriki kupiga kura hususan uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni kama kupoteza muda na sio hadhi yao,nawaomba sana mshiriki kwenye uchaguzi huu.Mhe. Simbachawene amesisitiza
Amesema suala la uchaguzi wa viongozi ni jukumu la wananchi wote wakiwemo Watumishi wa Umma
Naye, Mwenyekiti wa SHIMIWI Daniel Mwalusamba amesema jumla ya Watumishi 2995 wameshiriki kwenye michezo hiyo mwaka huu
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwashukuru Viongozi mbalimbali waliojitoa kwa hali na mali katika kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa