Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. SIMBACHAWENE AWATAKA WAAJIRI KATIKA TAASISI ZA UMMA KUIMARISHA USAWA NA KUONDOA UBAGUZI MAHALI PA KAZI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ametoa rai kwa Waajiri wote katika taasisi za umma kusoma, kuelewa na kutumia kikamilifu Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Jinsia na kuzingatia masuala ya Jinsia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema hayo wakati wa  tukio la uzinduzi wa Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma na Ufunguzi wa Mafunzo ya Wanawake Awamu ya Tatu na Nne yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Serikali ya Finland leo tarehe 16 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es salaam.

Mhe. Simbachawene ameilekeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kusambaza mwongozo huo kwenye mamlaka zote za ajira katika Utumishi wa Umma na kushirikiana na Mamlaka  hizo kuendesha mafunzo ili kuimarisha usawa na hatimaye kuondoa aina zote za ubaguzi mahali pa kazi.

“Ninawaelekeza waajiri wote katika taasisi za umma kuandaa Mpango kazi wa namna ya kutekeleza afua za usimamizi wa masuala ya jinsia mahala pa kazi na kutenga bajeti kwa kila mwaka wa fedha ili kumuwezesha Mratibu wa masuala ya Jinsia wa Taasisi husika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na uratibu wa mafunzo ya Jinsia katika Utumishi wa Umma kwenye Taasisi husika” alisisitiza Mhe. Simbachawene.

Vilevile, amemuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI kushirikiana na Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuzifikia Mamlaka zote za Mikoa 26 na Mamlaka za Serikali za Mitaa 184 ili kutoa mafunzo kuhusu Mwongozo huo ili kila mtumishi wa umma apate uelewa wa kutosha na kuepuka kuwa na ubaguzi mahali pa kazi.

Vile vile, Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa ili Taifa liweze kufikia usawa wa kijinsia, hasa kwenye masuala ya uongozi, hakuna budi kushirikisha wanaume katika utekelezaji wa mipango na jitihada mbalimbali za kufanikisha azma za wanawake kuwa viongozi.

“Kila mmoja anaona kuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara na mfano wa kuigwa katika kuinua wanawake na ameendelea kujipambanua katika uimarishaji wa haki na uwezeshaji wa wanawake kwa kuwateua na kuwapatia nafasi za uongozi.

Amesema amefurahi kuona wanaume pia wamealikwa kwenye kongamano hilo na baadhi ya wakufunzi kwenye programu hiyo ni wanaume.  Hivyo, ameitaka Taasisi ya UONGOZI kuendelea kuwashirikisha na kuwahusisha kikamilifu wanaume kwenye programu hii ili kuleta matokeo yenye tija.

Mhe. Simbachawene alihitimisha hotuba yake kwa kutoa shukrani za dhati kwa wadau wa maendeleo wakiwemo Serikali ya Finland, Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN WOMEN) kwa kuendelea kuiwezesha Taasisi ya UONGOZI kifedha na kiutaalamu (Financial and Technical Support) katika kutimiza majukumu yake kuwajengea uwezo viongozi hususan wanawake.

Naye, Katibu Mkuu – UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amesema Mwongozo huo unalenga kuweka mazingira bora na wezeshi ya ujumuishwaji wa jinsia katika Utumishi wa Umma ili kuongeza tija katika utendaji kazi na kuimarisha masuala ya haki na usawa kati ya Wanaume na wanawake kwa ngazi zote katika Utumishi wa Umma.

“Kupitia mwongozo huo, tunataka kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika nafasi za Uongozi na maamuzi ikiwa ni kipaumbele cha Serikali kuendeleza wanawake na kuwajengea uwezo na kujiamini katika utekelezaji wa majukumu yao” ameongeza.

Bw. Mkomi amebainisha kuwa, azma ya Serikali kupitia lengo namba tano (5) la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 kuhusu kufikia Usawa wa Kijinsia asilimia 50 katika uongozi, hivyo pamoja na jitihada za Ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma ambazo zimeendelea kufanywa na Serikali, bado baadhi ya Taasisi za Umma hazijaweza kujumuisha kikamilifu masuala ya Jinsia katika mipango na bajeti za Taasisi husika.

Ameongeza kuwa, uandaaji wa Mwongozo huo umepita awamu zote muhimu na kushirikisha kikamilifu wadau mbalimbali ikiwemo Wakurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara zote ambao walitoa maoni yao.