Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. SIMBACHAWENE AWATAKA VIONGOZI WA TAKUKURU KUBADILI CHANGAMOTO KUWA FURSA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (TAKUKURU) kutafakari kwa kina na kujadili changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi na kuzifanya kuwa fursa kwa maendeleo ya Taifa.

Mhe. Simbachawene amesema hayo leo tarehe 20 Novemba, 2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU-2023 katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma.

“Ninaamini mtatumia fursa ya mkutano huu wa mwaka kujadili masuala yote yanayoonekana kuwa ni changamoto katika utendaji kazi ili kupata suluhu ya pamoja” ameongeza Mhe. Simbachawene.

Aidha, katika hotuba yake amebainisha kuwa kila mmoja katika mazingira tofauti na kwa namna ya pekee ameruhusu au ameathiriwa na rushwa, hivyo ametoa rai kwa wananchi wote kuhakikisha wanazuia mianya ya rushwa ili kutoathiri vizazi vijavyo.

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa TAKUKURU inatakiwa kuitumia vizuri programu iliyoianzisha ya TAKUKURU Rafiki kwa lengo la kupanua wigo na kuwashirikisha wananchi katika kupambana na rushwa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema ofisi yake inaendelea na utekelezaji wa shughuli zake kwa mujibu wa Sheria na sasa wamejikita zaidi katika kuzuia rushwa.

“Tunaendelea na kazi ya kuelimisha umma kuhusu masuala ya rushwa na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Serikali ambapo tumeokoa fedha nyingi ambazo kama isingekuwa TAKUKURU basi fedha hizo zingeishia mikononi mwa watu binafsi” amesema Bw. Hamduni.

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubainisha changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi wao na kutafuta ufumbuzi wa pamoja. Mkutano huu wa Mwaka kwa mwaka 2023 una kaulimbiu ya Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu.