Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. SIMBACHAWENE ASISITIZA WAAJIRI KUSIMAMIA HAKI ZA WATUMISHI WANAOWASIMAMIA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kushirikiana na Wakuu wa Taasisi zao kuhakikisha watumishi wa Umma wanapata haki zao za kiutumishi kwa wakati bila kuhangaishwa ili waweze kutulia katika vituo vyao vya kazi na kutekeleza kikamilifu majukumu yao ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Ninawapongeza waajiri wote wanaowalinda watumishi wao ili rasilimali hiyo iweze kufanya kazi kwa ukamilifu na ufanisi, kwani bila hao hakuna chochote kitakachoweza kufanyika,” Mhe. Simbachawene amesisitiza na kutoa rai kwa wakuu hao kuzingatia misingi ya Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali katika Utumishi wa Umma na kuhakikisha watumishi wa Umma walio katika Taasisi zao wanatekeleza wajibu wao ipasavyo ili Serikali iweze kupata tija ya uwepo wao.

Mhe. Simbachawene amesema Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu ndio wasimamizi wa watumishi hivyo wasipowasaidia katika kutatua changamoto zao za kiutumishi ni sawa na uhujumu uchumi.

Ametoa siku 14 kuanzia leo kwa Wakuu wa Idara hizo kufanyia kazi changamoto za kiutumishi yakiwemo madai ya malipo mbalimbali ya watumishi na kuwasilisha kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI na taarifa ya jinsi walivyoshughulikia changamoto hizo.

“Katibu Mkuu, natoa siku 14 kuanzia leo, tupate taarifa ya namna madai ya malipo mbalimbali ya watumishi yalivyoshughulikiwa kwani tunatakiwa tutatue changamoto za watumishi hawa ili wawahudumie wananchi kwa furaha,” Mhe. Simbachawene ameongeza.

Pia, amesisitiza kuhusu uzingatiaji wa maadili kwa kuwa ofisi yake imeendelea kupokea malalamiko kuhusu vitendo vya uvunjifu wa maadili ikiwemo rushwa, lugha zisizofaa, kufanya udanganyifu wa nyaraka ikiwemo kughushi barua za masuala mbalimbali ya kiutumishi kama uhamisho wa kwenda sehemu zenye maslahi mazuri. Hivyo, ametoa wito kwa watumishi wote wanaojihusisha na tabia hiyo kuacha mara moja na hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa wahusika.

Vilevile, aliwaekeleza baadhi ya Waajiri kuacha tabia ya kukataa kuwapokea watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi zao na baadhi kutoruhusu watumishi kuhama hata pale inapoelekezwa na Mamlaka. “Suala hili ni kinyume na sheria, kanuni na taratibu kwa kuwa kitendo hicho ni kukosa utii kwa Serikali pamoja na Mamlaka zilizo juu yao,” Amesisitiza

Akitoa maelezo ya awali kuhusu lengo la kikao kazi hicho, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amesema kikao hicho kinajadili changamoto zinazoendana na utekelezaji wa majukumu ya utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu na namna bora ya kukabiliana nazo.

Ameongeza kuwa, washiriki watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuelimishana kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kushughulikia masuala mbalimbali ya utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma ili kuimarisha na kuboresha utendaji kazi kwa madhumuni ya kutoa huduma zenye tija kwa taifa na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa kiwango kinachotarajiwa.

Kikao kazi hicho cha siku tatu kimeandaliwa mahususi kwa lengo la kutathmini nafasi ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala katika kuwezesha utendaji wa taasisi na utumishi wa umma kwa jumla.