Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. SIMBACHAWENE AMEITAKA eGA KUKUZA VIPAJI NA UBUNIFU WA VIJANA KATIKA TEHAMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka Wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika eneo la TEHAMA kujifunza kwa bidii ili kupata ujuzi utakaoisaidia Serikali kutoa huduma kwa Umma kupitia TEHAMA kwa ufanisi, urahisi na gharama nafuu.

Mhe. Simbachawene amesema hayo tarehe 18 Septemba, 2023 wakati wa ziara yake fupi ya kutembelea Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji Mifumo ya TEHAMA cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kilichopo Chuo Kikuu Cha Dodoma ambapo alipata wasaa wa kuongea na wanafunzi hao waliotoka vyuo mbalimbali hapa nchini.

“Nimefurahi kuona ubunifu na vipaji vyenu na sasa ninaelekeza uongozi wa eGA kujenga na kuweka mazingira yenye uwezo wa kuchukua vijana wengi zaidi wenye vipaji na wabunifu kwenye eneo la TEHAMA ili waweze kufanya majaribio ya bunifu zao na kujiendeleza kwa vitendo kwa maendeleo ya taifa” alisema Mhe. Simbachawene.

Aidha, Serikali inafanya jitihada za kuboresha Utafiti na Ubunifu ili kujimarisha kwenye eneo la TEHAMA na kutoa huduma zake kwa ufanisi, urahisi na gharama nafuu. Serikali imeipa sekta ya TEHAMA kipaumbele, hivyo amewataka wanafunzi hao kuongeza bidii katika kujifunza ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwa na uwezo wa kujiajiri wenyewe.

Vilevile, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya UTUMISHI wa Umma Bw. Nolasco Kipanda amesema Ofisi ya Rais-UTUMISHI iko tayari kushirikiana na eGA kuangalia namna bora ya kuendelea kutumia vijana hao wanaoonekana kuwa na uwezo mkubwa katika masuala ya ubunifu wa mifumo ya TEHAMA.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Eng. Benedict Ndomba  amefafanua kuwa Mamlaka inatekeleza programu ya kukuza bunifu kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kutokana na vijana hao, Mamlaka imetengeneza mfumo wa eMikutano unaowezesha kufanya mikutano kwa njia ya mtandao (Video Conference), eDodoso kwa ajili ya kukusanya data na kuzichakata kupitia mtandao na mfumo wa eMrejesho unaowezesha wananchi kuwasiliana na Serikali yao moja kwa moja.