Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE: SIMBACHAWENE AISISITIZA IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA KUSIMAMIA UTENDAJI KAZI WA MASJALA SERIKALINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amesisitiza Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuendelea kuwa karibu zaidi na masjala za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuimarisha utendaji wa masjala hizo kwa utoaji wa huduma bora kwa umma.

Mhe. Simbachawene amesema masjala hizo zina hali isiyoridhisha na nyaraka hazihifadhiwi ipasavyo, hivyo Idara hiyo inatakiwa kutekeleza jukumu lake la kusimamia kumbukumbu na nyaraka na kuhakikisha viwango na miongozo inazingatiwa na taasisi zote umma.

“Kazi ya Serikali Kuu ni kupeleka miundombinu na rasilimaliwatu katika maeneo ambayo Mamlaka hizo zimeshindwa kutekeleza baadhi ya shughuli zake kutokana na kuweka vipaumbele katika sekta nyingine. Hivyo, andaeni mpango ambao unaweza kutumika kuomba fedha kwa ajili ya kujenga masjala nzuri katika ofisi za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa manufaa ya vizazi vijavyo” ameongeza Mhe. Simbachawene.

Aidha, amebainisha kuwa moja ya majukumu ya Idara hiyo ni kukusanya, kutunza, kuhifadhi na kuteketeza nyaraka kwa mujibu wa taratibu. Hivyo, ni lazima Idara hiyo ifanye kazi kwa karibu na masjala za Sekretarieti za Mikoa na zile za Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuleta ufanisi.

Pia, Mhe. Simbachawene ameelekeza idara hiyo kujenga kituo cha kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka katika Mkoa wa Mtwara ikiwa ni utekelezaji wa agizo la mtangulizi wake Mhe. George Mkuchika ili kulinda historia ya kanda ya kusini.

Mhe. Simbachawene amehitimisha ziara yake fupi ya kikazi tarehe 5 Disemba, 2023 katika ofisi za Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam.