Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. SIMBACHAWENE AHIMIZA UKAMILISHAJI WA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amepongeza uongozi na menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kazi nzuri ya usimamizi wa ujenzi wa chuo hicho  Kampasi ya Singida.

Salaamu hizo za pongezi amezitoa wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa chuo hicho tarehe 22 Mei, 2024 Mkoani Singida.

“Nimefika hapa Singida nimeona kazi inayoendelea na nimefurahishwa na kiwango na kasi ya ujenzi wa majengo haya ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa watumishi wa umma na umma kwa jumla” amesema Mhe. Simbachawene.

Aidha, ameonesha umuhimu wa chuo hicho na kuahidi kuelekeza viongozi wengine katika Ofisi anayoisimamia kupita na kukagua maendeleo ya mradi huo mara kwa mara kwa lengo la kuongeza hamasa ya ukamilishaji wa majengo hayo yanayotarajiwa kuanzia kutumika Novemba 2024.

Pia, Mhe. Simbachawene ameelekeza uongozi wa chuo hicho kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi na hosteli ili kuongeza motisha kwa watumishi na wanachuo mtawalia kuwa tayari kukaa katika eneo la chuo.

Halikadhalika, Mhe. Simbachawene ameipanda mti wa kumbukumbu katika Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida na kuelekeza uongozi wa chuo kupanda miti mingi katika eneo hilo ambalo linaonekana kuwa na upepo mkali.

Kazi ya ujenzi wa chuo cha utumishi kampasi ya Singida inaedelea na ujenzi umefikia asilimia 75 ambapo  Chuo cha Ufundi Arusha kina nafasi ya mshauri mwelekezi.