Habari
MHE. SANGU AHIMIZA MAFUNZO YA UONGOZI KWA BODI MBALIMBALI

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu ameitaka Taasisi ya Uongozi kuweka kipaumbele kwenye mafunzo yanayohusisha wajumbe wa bodi mbalimbali za Mashirika ya Umma ili kujenga uelewa mpana wa masuala ya kiuongozi ili wanapofanya uamuzi wowote wazingatie maslahi mapana ya Taifa.
Mhe. Sangu ametoa rai hiyo leo tarehe 16 Agosti, 2024 jijini Dar es salaam wakati alipofanya ziara ya kujifunza namna taasisi hiyo inavyofanya kazi na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi.
“Nimefarijika sana kusikia kuwa Taasisi ya Uongozi inatoa mafunzo mahususi ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji viongozi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania ikiwa pia ni sehemu ya utekelezaji wa jitihada za kuimarisha utawala bora”
Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada za kujenga nchi yetu katika nyanja mbalimbali, hivyo hatuna budi kumuunga mkono kwa kufanya mafunzo ambayo yanaweza kuwafanya viongozi mbalimbali kuwa wazalendo na wenye kiu ya kuona taifa linapata maendeleo.
Vile vile, amesisitiza watumishi wa Taasisi hiyo kuendelea na mshikamano katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa jukumu la kutoa mafunzo kwa Viongozi ni kubwa na linahitaji mshikamano.
Mhe. Sangu amefanya ziara katika Taasisi ya Uongozi kwa kwa lengo la kujifunza kuhusu majukumu ya Taasisi hiyo ambayo ipo chini ya Ofisi anayoiongoza.