Habari
MHE. RIDHIWANI KIKWETE AWAKUMBUSHA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA KUZINGATIA WAJIBU WAO WA KUSIMAMIA MAADILI BILA UPENDELEO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – UTUMISHI na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ametoa wito kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na bila upendeleo kwa kiongozi yeyote.
Akizungumza wakati akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba kwa ajili ya kuzungumza na watendaji wa Sekretarieti hiyo, Mhe. Kikwete amesisitiza umuhimu wa chombo hicho katika kusimamia maadili kwa kuzingatia misingi ya sheria, uwazi, ukweli na usawa, ili kuendelea kujenga taswira njema ya utumishi wa umma nchini.
Ameeleza kuwa viongozi wa umma wana wajibu mkubwa kwa jamii, hivyo ni muhimu Sekretarieti hiyo kutekeleza dhima yake ya kisheria ya kuhakikisha viongozi wote wanazingatia miiko na maadili katika kutekeleza majukumu yao.
“Hatuwezi kuwa na Serikali ambayo viongozi wanalalamikiwa kwamba ni wapotofu wa Maadili na sisi kama chombo cha kusimamia Maadili ya Viongozi wa Umma tumekaa kimya” Waziri Kikwete alisema.
Aidha, ametoa rai kwa watumishi wa Sekretarieti ya Maadili kuimarisha ushirikiano, kuendesha uchunguzi kwa haki bila upendeleo na kutoa elimu ya kutosha kuhusu maadili kwa viongozi wa umma na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wao, watendaji wa Sekretarieti hiyo wamemhakikishia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – UTUMISHI Mhe. Ridhiwani Kikwete kuwa wataendelea kufanya kazi kwa kuzingatia uwajibikaji, uadilifu na weledi ili kuimarisha imani ya wananchi katika mifumo ya utawala bora.